Jeshi la polisi limewatawanya viongozi wa chadema kwa mabomu ya machozi. - KULUNZI FIKRA

Friday 16 February 2018

Jeshi la polisi limewatawanya viongozi wa chadema kwa mabomu ya machozi.

Mwenyekiti wa chadema Taifa, Mhe Freeman Aikael Mbowe, na Salum Mwalim ambaye ni mgombea ubunge wa Chadema katika Jimbo la Kinondoni wameapa kukabiliana na mtu yoyote atakayejaribu kuhujumu uchaguzi utakaofanyika kesho.

Mhe Mbowe amesema Tume ya Uchaguzi kupitia Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni imekuwa ikijaribu kufanya hujuma kwa chama chake ikiwemo kutotoa fomu za viapo kwa mawakala wa Chadema watakaosimamia uchaguzi, kesho Jumamosi.

Kwa upande wake Salum Mwalim, ambaye ni mgombea wa chama hicho amesema, amesema “Walahi walahi, naapa siku ya kesho kama kuna mtu atahujumu uchaguzi, nitakufa naye nikipigania haki ya wananchi wa Kinondoni.

Baba yangu alikufa akiwa analinda mipaka ya nchi hii akiwa na miaka 38 na kuniacha nikiwa na miaka mitano, na mimi kama wakitaka kuhujumu uchaguzi nitakufa kwa kupigwa risasi nikiwa natetea haki ya wananchi kuchagua kiongozi wanayemtaka.”

Mhe Mbowe amesema, “Wanashindwa kuongoza, wananunua wajinga, wanaua viongozi, wanateka wasaidizi wetu. Ben Saanane kosa lake ni nini? Aliandika makala akiuliza uhalali ya digrii ya Rais inayoitwa PhD.”

Baada ya mkutano huo uliofanyika viwanja vya Buibui Kinondoni wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara waliamua kutembea kuelekea Magomeni, ofsisi ya mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni baada ya Mbowe kuwaeleza kuwa msimamizi huyo wa uchaguzi amegoma kutoa fomu za viapo vya mawakala wa chama hicho kwa ajili ya uchaguzi wa kesho.

Viongozi wa juu wa Chadema akiwemo Mhe Mbowe, Katibu Mkuu Dkt Vincent Mahinji, Mbunge wa Jimbo la Kawe Mhe  Halima Mdee, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho, Naibu Katibu Mkuu bara Mhe John Mnyika, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mhe  John Heche, mgombea ubunge Salum Mwalim na wengineo pia walikuwa sehemu ya wananchi waliokuwa wakitembea kuelekea Magomeni, zilizopo ofisi za mkurugenzi wa manispaa.

Baada ya wananchi na viongozi wa Chadema kutembea kwa miguu kutoka uwanja wa Buibui, mpaka Mkwajuni, askari polisi wakiwa katika magari zaidi ya matano waliweka kizuizi na kuanza kupiga mabomu kuwatawanya wananchi hao.

Katika hekaheka hizo, mwandishi  wetu alishuhudia wananchi zaidi ya 30 wakitiwa nguvuni huku baadhi yao wakijeruhiwa vibaya kwa vipigo kutoka kwa askari waliojihami kwa silaha za moto.

Kufuatia vipigo vizito kwa baadhi ya wananchi, askari hao waliita gari ya kubebea wagonjwa (ambulance), ambayo ilibeba baadhi ya watu na kuondoka nao kuelekea eneo ambalo halikufahamika mara moja na mwandishi.

Kampeni za uchaguzi wa mbunge wa jimbo la Kinondoni zimehitimishwa leo, huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika kesho, Jumamosi ya 16 Februari, 2018. Uchaguzi unafanyika ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Maulid Mtulia, aliyejiuzulu nafasi hiyo, kukihama chama cha CUF na kutimkia CCM, ambacho kimemsimamisha tena kuwania nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment

Popular