Mambo matano yaliyotikisa vikao vya Bunge. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 11 February 2018

Mambo matano yaliyotikisa vikao vya Bunge.

 
Licha ya Mkutano wa 10 wa Bunge la 11 uliomalizika juzi kuwa mahsusi kwa ajili ya kamati za kudumu kuwasilisha taarifa zake ambazo hufuatiwa na mijadala mizito hasa ya ufisadi, safari hii haikuwa hiyo pekee kwani kuna mambo matano makubwa yaliyoibuka na kutikisa chombo hicho, baadhi yakiwa hayatokani na taarifa hizo.

Katika mkutano huo uliofanyika kwa siku 12 na kumalizika juzi, kamati zilizowasilisha taarifa zake ni; Hesabu za Serikali (PAC); Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC); Bajeti; Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC); Viwanda, Biashara na M|azingira.

Nyingine ni Kamati ya Ardhi, maliasili na utalii; Kilimo, Mifugo na Maji; Miundombinu; Katiba na Sheria; Utawala na Serikali za Mitaa; Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Mambo yaliyotikisa bungeni ni mradi wa hati ya kielektroniki ya kusafiria, fao la kujitoa, wabunge kutaka ulinzi, uhaba wa maji na utendaji wa baadhi ya mawaziri.

Hati za kusafiria

Januari 30, Rais John Magufuli alizindua hati za kielektroniki za kusafiria jambo ambalo liliibuka bungeni baada ya baadhi ya wabunge kueleza kuwa mradi huo umegubikwa na ufisadi.

Mbunge wa Momba (Chadema), Mhe David Silinde alisema taarifa zinaonyesha kuwa ufisadi ndani ya nchi bado umeendelea kuwapo na kwamba mradi huo umekuwa ukitekelezwa kwa gharama za Dola 40 milioni za Marekani.

“Kuna taarifa nimezipata kuwa mradi huo ulikuwa na thamani ya dola 16 milioni za Marekani sawa na paundi 11 milioni. Kuna taarifa kwamba kampuni ambayo ilishapewa hati ya makubaliano ambayo hayakusainiwa hadi dakika ya mwisho, lakini mwisho wa siku ilipewa kampuni ya HID,” alisema Mhe Silinde.

Alisema kampuni ya HID ambayo imepewa tenda hiyo haijawahi kufanya kazi ya mradi wa hati za kusafiria mahali popote na imekuwa ikitengeneza kadi.

Alisema kampuni hiyo imeingia ubia na watu ambao walikuwa Nida (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa) wakati uliopita.

“Kwa hiyo mheshimiwa mwenyekiti, ufisadi bado upo na uchumi umeendelea kuyumba lakini watu wameendelea kufichaficha tu kwa namna fulani, kama tunapinga ufisadi lazima hatua zichukuliwe,” alisema.

Alisema taarifa walizonazo za ndani katika mradi wa hati za kusafiria kuna ufisadi wa kutisha.

Mbali na Mhe Silinde suala hilo lilizungumziwa pia na Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), Mhe John Heche na mwenzake wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ambaye alitakiwa na Naibu Spika, Dkt Tulia Ackson kuwasilisha nyaraka za ushahidi kuhusu ufisadi wa mradi huo wa hati za kusafiria kwa kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge.

Fao la kujitoa

Uliibuka mjadala mkali wa Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa mwaka 2017, huku kambi ya upinzani bungeni ikipendekeza Serikali kuweka fao la kujitoa kutokana na umuhimu wake.

Muswada huo unalenga kuunganisha mifuko mitano ya hifadhi ya jamii na kuwa na miwili kwa ajili ya watumishi wa umma na sekta binafsi. Mifuko iliyopo sasa ni LAPF, PPF, GEPF, PSPF na NSSF na itakayobaki ni NSSF na PSPF.

Mbunge wa Bunda (Chadema), Mhe Ester Bulaya alisema kambi hiyo inaona umuhimu mkubwa wa kuwapo kwa fao la kujitoa kama lilivyokuwa linatolewa na mifuko iliyokuwapo.

“Bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na fao la kujitoa kama lilivyokuwa linatolewa na mifuko iliyokuwapo. Bado ni la msingi na lazima kwani mwanachama anakuwa tayari na akiba yake hivyo inakuwa ni mtaji wa kumtoa kwenye umaskini wa kipato,” alisema Mhe Bulaya.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Mhe Zitto Kabwe alisema hakuna namna ya kuendelea kulikwepa fao hilo kama ilivyokuwa kwa miaka minne iliyopita.

“Huko nje vijana wengi sana wanataka fao hili liwepo, dhamira ya Serikali na dola yoyote ni kujenga mazingira ambayo mfumo madhubuti wa hifadhi ya jamii ambao hautakufanya baadaye uwe na wazee ambao hawana pensheni,” alisema Mhe Zitto kabwe.

Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Mhe  Constatine Kanyasu alisema anatoka katika mkoa ambao una wachimbaji wa madini wengi na mgogoro wake mkubwa siku nyingi umekuwa ni fao la kujitoa.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri wa Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alisema hakuna nchi yoyote ambayo mifuko ya jamii ina fao la kujitoa lakini Serikali kwa kutambua umuhimu huo, imeweka fao la upotevu wa ajira.

Wabunge kuomba ulinzi

Siku ya mwisho ya mkutano huo, Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilipendekeza kufanyiwa marekebisho Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ili kuweka sharti la wabunge kupatiwa ulinzi katika maeneo mbalimbali.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Balozi Adadi Rajabu alisema ulinzi huo uwe katika makazi ya wabunge wakiwa wanatekeleza majukumu ya kibunge mjini Dodoma na katika majimbo yao.

Mapendekezo ya kamati hiyo yalionekana kuwagusa wabunge wengi baada ya mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa wakati akichangia taarifa hiyo kutoa mfano wa tukio la kupigwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na hivyo kupendekeza wabunge walindwe.

Mbunge wa Mtama (CCM),  Mhe Nape Nnauye alitaka Sheria ya Usalama wa Taifa ifanyiwe marekebisho kwa kuwa inazungumzia ulinzi wa viongozi na si wananchi wengine.

Wakati Dkt Tulia, akiagiza Serikali kulifanyia kazi suala la ulinzi na uwekaji wa namba maalumu kwa magari ya wabunge kama ilivyopendekezwa na kamati, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dkt Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Mhe George Mkuchika walipangua hoja za mapendekezo ya kamati hiyo kuhusu ulinzi wa wabunge na kuhusishwa na yale yaliyohusu idara ya Usalama wa Taifa.

Hoja ya kukosekana kwa maji

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe Isack Kamwelwe alijikuta katika wakati mgumu baada ya wabunge wengi kumbana wakitaka majibu ya maji kutokana na hoja ya dharura ya mbunge wa Nzega (CCM),  Mhe Hussein Bashe.

Katika hoja yake, Mhe  Bashe aliwashtaki mawaziri bungeni akisema wamekuwa chanzo cha mateso na mahangaiko kwa wananchi wa Nzega lakini akasema lolote litakalotokea walaumiwe wao.

Mhe Bashe aliwataja mawaziri hao kuwa ni Dk Philip Mpango (Fedha), Mhe Dkt Medrad Kalemani (Nishati), Kamwelwe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo kwamba wamesababisha wananchi wa jimbo lake kukosa maji kwa siku ya 13 mfululizo.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo alipoomba mwongozo akitumia kanuni ya 47 kuhusu jambo la dharura bungeni na alipopewa nafasi alisema amekuwa akiwasiliana na Serikali lakini hakuna kinachoendelea na wahusika wamekaa kimya.

Hoja yake ilimuinua Mwenyekiti wa Bunge, Mhe Andrew Chenge aliyesema tatizo la maji ni la nchi nzima na kwamba halitakiwi kupuuzwa na kutaka wananchi watendewe haki maeneo yote.

Licha ya Waziri Mhagama kuagiza mawaziri wa Maji, Nishati na Fedha kukutana mara baada ya kikao cha Bunge kuahirishwa, jambo hilo liliendelea kutikia Bunge

Mbunge wa Nchemba (CCM), Mhe Juma Nkamia naye alieleza ukubwa wa tatizo hilo katika jimbo lake huku mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete akieleza jinsi anavyojibiwa kisiasa na waziri Kamwelwe kuhusu maji.

Hata hivyo, Mhe Chenge alizima moto wa wabunge hao baada ya kusema Serikali imeyachukua maoni yao na itayafanyia kazi.

Mawaziri na mihemko

Mawaziri wawili, Mhe Luhaga Mpina na Mhe Dkt Hamisi Kigwangalla walilazimika kutoa majibu ya kina bungeni baada ya kushambuliwa kuhusu utendaji wao.

Mhe Dkt Kigwangalla anayesimamia Wizara ya Maliasili na Utalii na Mpina ambaye ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, walisema wataendelea kufanya kazi kwa weledi.

Mbunge wa Busega (CCM), Mhe Dkt Raphael Chegeni alimuweka Mpina katika wakati mgumu baada ya kusema amekuwa na kiburi na kumtaka aache kwa kuwa anawaumiza wafugaji, akitolea mfano kamatakamata ya mifugo.

Mhe Nape alisema hakuna lililofanyika kwa wafugaji tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulipomalizika na kwamba kila wakati Serikali inafanya kazi ya zimamoto badala ya kujipanga na kushughulikia matatizo ya wananchi kikamilifu.

Mbunge wa Chambani (CUF), Mhe Yusuph Salum Hussein, alisema Wizara ya Maliasili na Utalii ni kama yai viza ambalo lina matumizi mazuri kwa wanaolitumia lakini likikosewa linanuka.

Mchungaji  Peter Msigwa naye aligusia wizara hiyo, kubainisha kuwa Kamati ya Maliasili imepokea malalamiko kutokana na hatua ya waziri Kigwangalla kufuta vitalu vya uwindaji.

No comments:

Post a Comment

Popular