Makonda apokea kero nzito. - KULUNZI FIKRA

Saturday, 10 February 2018

Makonda apokea kero nzito.

Marehemu kutoacha wosia, sheria ya dini ya Kiislamu kutomtambua mtoto wa nje ya ndoa na kutofungua mirathi mapema kumetajwa kuwanyima haki wanufaika wa mirathi.

Hayo yameelezwa leo Februari 10, 2018 katika ukumbi wa Diamond Jubilee katika mkutano unaoendelea muda huu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kupokea taarifa ya malalamiko ya wananchi yaliyowasilishwa kwa wanasheria wa mkoa huo.

Akiwasilisha taarifa ya siku sita za kusikiliza malalamiko ya wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam, mwanasheria Siraji Shabani amesema wamepokea malalamiko 87, kati ya hayo 40 yalikuwa mahakamani na 47 hayajafikishwa mahakamani kutokana na wahusika kutokuwa na elimu ya namna sahihi ya kufungua kesi za mirathi.

Shabani amesema changamoto kubwa waliyokutana nayo ni marehemu kutoacha wosia wa kisheria na kusababisha familia kushindwa kupata suluhisho la mali zilizoachwa.

“Mke na watoto iwapo mume amefariki ndiyo huwa waathirika wakuu wa mali za marehemu ambapo hudhulumiwa na ndugu wa familia ya marehemu,” amesema Shabani.

Ameitaja changamoto nyingine ni wanafamilia kutofungua mirathi kwa wakati na kusababisha kupitwa na wakati.

Amesema changamoto nyingine ni mwingiliano wa maisha ambapo watoto wa nje ya ndoa kukosa haki ya kurithi kutokana na dini ya Kiislamu kutomtambua mtoto wa nje ya ndoa.

“Nashauri kuwapo utaratibu wa kuandika wosia, urithi kabla ili kuondoa mkanganyiko huu iwapo mmoja wa wanafamilia anapofariki,” amesema,

“Wanafamilia wawe waaminifu katika kusimamia mirathi ya jamaa zao ili kuwapatia haki watoto wa marehemu badala ya kutumia mwanya huo kuwadhulumu.”

Malalamiko hayo pamoja na mengine yatawasilishwa kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment

Popular