Jeshi la polisi limekiri kumpiga mtu mmoja Risasi katika maandamano ya Chadema. - KULUNZI FIKRA

Saturday 17 February 2018

Jeshi la polisi limekiri kumpiga mtu mmoja Risasi katika maandamano ya Chadema.

 
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amekiri mtu mmoja kupigwa risasi na polisi wakati wakiwatawanya wafuasi wa Chadema walioandama jana Februari 16, 2018.

Wafuasi hao wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliandamana kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aron Kagurumjuli kudai viapo vya mawakala wa chama hicho.

Maandamano hayo yalianzia viwanja vya Buibui Mwananyamala ulikokuwa ukifanyika mkutano wa kampeni wa Chadema na yalipofika eneo la Mkwajuni wafuasi hao walitawanywa na polisi, huku mtu mmoja aliyekuwa kwenye basi la daladala akidaiwa kupigwa risasi na kufariki dunia.

Akizungumza na mwandishi wa habari wa kulunzifikra blog, Leo  Februari 17 Jumamosi, kamanda Mambosasa amesema “Walizuia mwendo kasi, wakaanza kupiga mawe kwa hiyo kati ya risasi za hewani zilizopigwa kuwatawanya kuna iliyompata (mtu).”

Ufafanuzi huo wa kamanda Mambosasa licha ya kutoweka wazi kama mtu huyo amefariki dunia ama la, umekuja huku ikidaiwa kuwa aliyepigwa risasi na kupoteza maisha ni mwanafunzi wa elimu ya juu.

Taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo zilianza kusambaa tangu Ijumaa jioni katika mitandao ya kijamii sambamba na kuwekwa picha yake huku ikieleza kuwa amepigwa risasi wakati akiteremka katika basi.

Kamanda Mambosasa alipoulizwa kama mtu huyo ni mwanafunzi wa elimu ya juu amesema, “Haijathibitishwa hiyo, nipo kwenye pilika za uchaguzi, nadhani nitajibu hilo nitakaporejea ofisini na kupata taarifa.”

Uchaguzi wa majimbo ya Kinondoni na Siha unaendelea leo Jumamosi na Mwananchi litakuwa linakuletea kila kinachoendelea.

No comments:

Post a Comment

Popular