Fuvu la binadamu la miaka mia lakutwa kwenye ofisi ya Mawakili. - KULUNZI FIKRA

Friday 16 February 2018

Fuvu la binadamu la miaka mia lakutwa kwenye ofisi ya Mawakili.

 
Wajenzi wa jengo la ofisi ya kampuni ya uwakili jijini Dar es Salaam, wamekuta fuvu la binadamu linalosadikiwa kuwa la miaka 100 iliyopita.

Jengo linalojengwa upya ni mali ya Kampuni ya uwakili ya IMMMA, baada ya la awali kuharibiwa na mlipuko mwaka jana.

Mmoja wa mawakili wa kampuni hiyo, Fatuma Karume, aliiambia Nipashe jana kuwa baada ya jengo la ofisi hiyo kuharibiwa, walivunja jengo la nyuma yake kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya.

“Wakati mkandarasi anachimba chini ndipo walipokuta fuvu, inasemekana limezikwa kama miaka 100, nafikiri lilikuwa ni kaburi la mtu binafsi,” alisema.

Karume alisema kaburi lolote kulihamisha inabidi itolewa amri ya mahakama na mamlaka ya kushughulikia suala hilo ni polisi.

“Polisi watafanya kazi hiyo, sio kazi yetu kwa sababu hili kaburi linaonyesha ni la muda mrefu, tulichokuta ni fuvu,” alisema Karume.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamdani, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kueleza kuwa kichwa kinachodhaniwa cha binadamu kilikutwa urefu wa futi tatu hadi nne na mafundi hao.

“Tunafanya uchunguzi kubaini kama hivyo viungo ni vya binadamu na pia kuangalia historia ya eneo hilo,” alisema Hamdani.

“Tutakapojiridhisha kama ni viungo vya binadamu tutafuata taratibu za kisheria,” aliongeza Kamanda Hamdani bila kudokeza ni hatua zipi za kisheria.

No comments:

Post a Comment

Popular