Waziri wa Tamisemi atangaza neema. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 25 January 2018

Waziri wa Tamisemi atangaza neema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mhe Seleman Jafo amesema Serikali kwa sasa inatafuta Sh2 bilioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha.

Mhe Jafo aliyasema hayo jana katika viwanja vya Sanya Juu wakati akimnadi mgombea ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt Godwin Mollel, ambaye hivi karibuni alijiondoa Chadema na kugombea tena nafasi hiyo kupitia chama tawala.

Mhe Jafo alisema chama hicho ndicho chenye Serikali na ndicho kinachoweza kutatua changamoto na shida za wananchi.

Alisema endapo Dkt Mollel atashinda, Serikali itafanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha Siha inasonga mbele kimaendeleo na maisha ya wananchi yanaboreshwa.Jaffo aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua Dkt Mollel ili kuisukuma Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.

“Mollel ni kiongozi makini, mpeni ridhaa ili Serikali tushirikiane naye kuwaletea maendeleo na ninawahakikishia mkimchagua, miaka miwili iliyobaki Siha itakuwa moja ya wilaya ambazo zitapiga hatua kubwa na kufanya vizuri katika utekelezaji wa maendeleo,” alisema.

“Naomba msifanye makosa maana tutashughulika na shida na changamoto zote za wananchi, tutatatuta tatizo la maji, tutaboresha huduma za afya, elimu, barabara na kuwafanya wananchi kupata huduma zote muhimu za kijamii.”

Akimnadi Dkt Mollel, katibu wa itikati na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole mbali na kuwaomba wananchi wa Siha kumchagua Mollel aliwataka wanasiasa kuacha kutumia shida za wananchi kama mtaji wa kisiasa.

“Muda wa kufanya siasa za uwongo umepitwa na wakati, sasa tufanye siasa za kushughulika na shida za wananchi, tuboreshe maisha na kusogeza karibu na wananchi huduma za kijamii na tusigeuze maisha ya watu kuwa mtaji wa kisiasa,” alisema Polepole.

Polepole alisema maendeleo hayana vyama, hivyo kuwataka wananchi kumchagua Dkt Mollel, ambaye amehamia timu ya ushindi ambayo ina uhakika wa kuwaletea maendeleo.Akiomba kura, Dkt  Mollel alisema alivua gwanda ili aweze kushughulika na shida za wananchi na hivyo akawaomba wananchi kumpa kura zote za ndio.

Aliwaambia wananchi kuwa anatambua mchango wao wa mwaka 2015, hivyo wamrudishe ulingoni ili akatatue changamoto zinazowakabili, ambazo alishindwa kuzitatua akiwa upinzani.

“Natambua mchango wenu katika ubunge nilioupata 2015, lakini mlinituma kusoma ramani ya maendeleo na niliona nilikokuwa kulinituma katika ramani ya vijiweni na ndio maana nimeingia huku ambapo naona ramani ya maendeleo inasomeka vyema, hivyo nipeni kura zote ili nikatekeleze,” alisema Polepole.

Alisema akichaguliwa Februari 17,atashirikiana na Serikali kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili, ikiwemo tatizo la maji, miundombinu ya shule, barabara na migogoro ya ardhi.

No comments:

Post a Comment

Popular