Sugu na Emanuel Masonga kuanza kujitetea Leo. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 25 January 2018

Sugu na Emanuel Masonga kuanza kujitetea Leo.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na katibu wa Chadema wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga leo wanaanza kutoa utetezi wao katika kesi inayowakabili baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao jana.

Wawili hao watatumia mashahidi saba na vielelezo visivyopungua nane kujenga hoja dhidi ya mashtaka ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya. Wanatuhumiwa kutenda kosa hilo Desemba 30 mwaka jana wakiwa kwenye mkutano wa hadhara walioufanya kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Jana upande wa Jamhuri ulifunga ushahidi wake baada ya kuwapeleka mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti iliyorekodiwa na shahidi wa tano kwa kutumia mashine ya kurekodia ambayo ilisikilizwa mbele ya mahakama hiyo.

Wakili wa Mkuu Serikali, Joseph Pande aliiambia mahakama hiyo jana mchana baada ya shahidi wa watano, Inspekta Joram Magova kuwasilisha ushahidi wake kuwa wameleta mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti, hivyo hawana sababu ya kuita mashahidi wengine.

Baadaye, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite alitoa nafasi kwa mawakili wa utetezi, Hekima Mwasipu na Boniface Mwabukusi ambaye aliomba upande wao kuanza kutoa utetezi wao leo.

“Mheshimiwa hakimu, tunaomba upande wa utetezi tuanze kesho (leo) saa 4:00 asubuhi ili tupate muda wa kuzungumza na wateja wetu kwa kuwa wapo mahabusu hadi sasa. Na katika utetezi wetu tunatarajia kuwa na mashahidi saba na vielelezo visivyopungua nane,” alisema.

Awali, Hakimu Mteite alianza kwa kusoma uamuzi mdogo wa kusikilizwa ama kutosikilizwa kwa ushahidi wa sauti uliotolewa na shahidi wa tano ambao mawakili utetezi waliupinga kwa madai kuwa haukidhi matakwa ya kisheria.

Kutokana na ubishani huo, Hakimu Mteite aliahirisha kesi hiyo hadi jana asubuhi alipotoa uamuzi mdogo kuhusu ubishi huo kwa kusema mahakama yake imejiridhisha pasipo shaka kwamba hoja za mawakili wa utetezi hazina mashiko, hivyo inakubali sauti hiyo itumike ili kujua kilichozungumzwa na washtakiwa.

Tangu kesi nhiyo ianze, ulinzi umekuwa ukiimarishwa ndani na nje ya viwanja vya mahakama hiyo, lakini jana ulinzi ulionekana kuwa mkali zaidi askari walionekana kuwazuia wafuasi wa Chadema kuingia ndani ya mahakama hiyo na kuamriwa kukaa mbali na eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo, wafausi hao walilalamika hadi wakili wa utetezi, Mwabukusi kulazimika kwenza kuzungumza na askari hao ambao waliruhusu watu wachache kuingia kwa maelezo kuwa chumba cha mahakama ni kidogo.

Mbowe awatuliza wafuasi

Wafuasi hao pia walitulizwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyefika jijini Mbeya jana alfajiri na baadaye saa 3:00 asubuhi kufika mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.

Baadaye Mbowe alipata nafasi ya kuzungumza na wafuasi waliokuwa nje ya mahakama hiyo na kuwasihi kuwa watulivu kutokana na misukosuko wanayoipata, ikiwamo kuzuiwa kuingia ndani ya mahakama ili kupata fursa ya kusikiliza kesi hiyo na kuwataka wasiingie kama walivyoagizwa.

“Nawaomba sana ndugu zangu tuwe watulivu. Naamini mahakama itatenda haki tu,” alisema Mbowe.

“Tutaendelea kuongeza nguvu katika kesi hii ikibidi kuongeza mawakili wengine kuja kusaidiana na mawakili wetu hawa wanaoendelea hapa ili hatimaye haki inatendeka kwa viongozi wetu. Katika maeneo mengine huwa tunadai mahakama iwekwe utaratibu wa kufunga vipaza sauti nje ili watu hata wasipoingia ndani waweze kusikiliza kinachoendelea ndani.

“Sasa hili tumeona kuna upungufu, hivyo tunawasiliana na mawakili wetu ili kuona hili linafanyika na nyinyi muweze kupata haki yenu inayostahili.”

No comments:

Post a Comment

Popular