Gavana amuaga Rais Magufuli, amesema ameacha uchumi ukizidi kukua. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 4 January 2018

Gavana amuaga Rais Magufuli, amesema ameacha uchumi ukizidi kukua.

 
 RAIS wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ameagana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayemaliza muda wake, Profesa Benno Ndulu (pichani) Ikulu jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo yao jana, Profesa Ndulu alimshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kufanya naye kazi tangu alipoingia madarakani na amebainisha kuwa anafurahi kumaliza kipindi chake huku uchumi wa nchi ukiwa mzuri.

Alimpongeza kwa miongozo muhimu iliyosaidia kuimarisha uchumi, ikiwemo kudhibiti mfumuko wa bei ambao Novemba mwaka jana ulifikia asilimia 4.4 na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani bilioni 1.8 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 6 hivi sasa.

Hatua hiyo imedaiwa kuwa imeimarisha uwezo wa Serikali kujiendesha na kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo. “Nimekuja kumuaga Rais na kumshukuru, nafurahi kuwa naondoka wakati hali ya uchumi ikiwa nzuri, Taifa linakopesheka na kuna mazingira mazuri zaidi ya uchumi kuendelea kukua.

“Nampongeza sana Rais kwa kusimamia mambo mbalimbali muhimu ya kuimarisha na kukuza uchumi katika kipindi chote nilichofanya nae kazi,” alisema Profesa Ndulu. Rais Magufuli pia alizungumza na Gavana Mteule, Profesa Florens Luoga na baada ya mazungumzo hayo, alimshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi huo na kumhakikishia kuwa ataisimamia BoT ili iendelee kuwa chombo imara cha kusimamia uchumi wa nchi.

Kazi nyingine alizoahidi kuzifanya ni kuisimamia fedha ya Tanzania na kuhakikisha nchi inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wa jijini Dar es Salaam na mradi wa umeme katika maporomoko ya maji ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).

Profesa Luoga aliungana na Profesa Ndulu kueleza kuwa taarifa zinazotolewa na BoT kuhusu ukuaji wa uchumi, zinaandaliwa kitaalamu na kwa kushirikisha vyombo mbalimbali vikiwemo Benki ya Dunia (WB).

Vyombo vingine ni Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Alionya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipotosha ukweli kuhusu takwimu za uchumi, zinazotolewa na BoT. Kwa upande wake Rais Magufuli alimpongeza Profesa Ndulu kwa utumishi wake wa miaka 10 na kazi nzuri aliyoifanya kusimamia uchumi, ambapo katika kipindi hicho kasi ya ukuaji wa uchumi imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 5 hadi kufikia asilimia 7.

Ameimarisha usimamizi wa benki na maduka ya kubadilishia fedha, amesimamia ongezeko la akiba ya fedha za kigeni inayoiwezesha nchi kumudu kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi 6 na kuanza kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa reli, umeme, ununuzi wa ndege na mingine.

Ndulu aula tena “Nakushukuru sana Profesa Ndulu, umefanya kazi nzuri ya kusimamia uchumi wa Taifa letu, ndiyo maana leo unamaliza muda wako lakini tayari Benki ya Dunia na Kamisheni ya Dunia inayoshughulikia Teknolojia na Maendeleo Shirikishi wanakuhitaji ufanye nao kazi, na mimi nimeidhinisha uende ukatuwakilishe,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alimpongeza Gavana mteule, Profesa Luoga kwa kupokea uteuzi wake na alimtaka kufanya kazi ya kusimamia uchumi wa Taifa kwa ufanisi mkubwa zaidi ili nchi ipige hatua za maendeleo kwa kasi zaidi.

Ulipaji madeni ya ndani mwezi ujao Wakati huo huo, Rais Magufuli amesema mwezi ujao Serikali itatoa Sh bilioni 200 kwa ajili ya kulipa madeni ya ndani yatakayokuwa yamehakikiwa, yakiwemo ya wazabuni mbalimbali waliotoa huduma katika taasisi za serikali, madai ya walimu na madai ya wakandarasi.

“Nasisitiza madeni tutakayolipa ni ya ndani, na tutalipa madeni ambayo yamehakikiwa, kwa hiyo maandalizi ya kutoa fedha hizo yaanze mara moja na ni matarajio yangu fedha hizi zitasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wetu,” alisema

No comments:

Post a Comment

Popular