Tundu Lissu asimulia mambo mazito kwa Mara ya kwanza. - KULUNZI FIKRA

Friday, 1 December 2017

Tundu Lissu asimulia mambo mazito kwa Mara ya kwanza.

 
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesimulia hali ilivyokuwa siku ya tukio na pia kueleza ujumbe aliompa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipomtembelea hospitalini jijini hapa juzi.

Mbunge huyo, ambaye alishambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari lililoegeshwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7, pia amesema amepitia majaribu mengi, lakini “hili ndilo kubwa”.

Amesema hali yake inaendelea vizuri na madaktari wanamuelezea kuwa ni “muujiza unaoishi” baada ya kufanikiwa kuunganisha vipande vya mwili ulioharibiwa kwa risasi.

Lissu alisema hayo alipofanya mahojiano na chombo kimoja cha habari nchini, ikiwa ni mara ya kwanza kwa chombo cha habari cha Tanzania tangu ashambuliwe.

Lissu amelazwa Hospitali ya Nairobi jijini hapa tangu Septemba 7 na huenda akahamishiwa nje ya bara la Afrika kwa matibabu zaidi, ambayo yatahusu mazoezi, kabla ya kurejea nchini.

Akizungumza na chombo hicho, hospitalini hapo, Lissu alisema sasa anaamini kuwa Rais John Magufuli anajua kuna mgonjwa Nairobi na hivyo kufungua milango kwa wengine waliokuwa na hofu.

“Mimi namuamini na naendelea kuamini kwamba kwa sababu sasa Makamu wa Rais amekuja kwa niaba ya Rais, ametambua tuna mgonjwa yupo Nairobi. Milango itafunguka kwa wale wengine wote waliokuwa na hofu ya kuja,” alisema Lissu.

“Sasa Rais mwenyewe kamtuma makamu wake kuja kunipa pole, kwa hiyo hao wengine wa taasisi zote hawana hofu ya kuja kuniona.”

Akizungumzia mazungumzo yake na Suluhu, Lissu alisema yalikuwa mazuri.

“Mama Samia ni kiongozi wa kwanza wa Serikali ya Tanzania pamoja na mihimili yake kuja kunitembelea,” alisema Lissu.

“Spika wa Bunge hajaja, katibu wake na uongozi mzima wa Bunge haujaja. Jaji Mkuu au Jaji Kiongozi hawajaja pamoja na kwamba mimi ni Rais wa TLS.

“Na kwa kawaida mila na desturi za mahakama zetu, bila mawakili hakuna mahakama na kama Rais wa TLS nimekuwa nikialikwa na kuhudhuria vikao mbalimbali vya kiutendaji, lakini tangu nimeshambuliwa Jaji Mkuu au uongozi mzima wa Mahakama hata kutoa salamu za pole, hakuna.

“Rais Magufuli alikuwa hajawahi kusema lolote kuhusu kushambuliwa kwangu kama nakumbuka, lakini leo (juzi) amekuja Makamu wa Rais na amenieleza na napenda kuamini ni kweli ametumwa na Rais kama sehemu yake ya shughuli zilizomleta Kenya apitie kunisalimia na kunipa pole.”

Alisema Makamu wa Rais, ambaye waliwahi kufanya naye kazi wakati akiwa waziri anayehusika na Muungano na Lissu akiwa waziri kivuli wa eneo hilo, alimuuliza kama ana jambo lolote la kumweleza Rais, naye akamweleza kuhusu gharama za matibabu.

“Mimi bado ni mbunge, ujumbe ambao nataka aupeleke ni Bunge liko wapi? Bunge ambalo lina wajibu wa kisheria wa kunihudumia nikiwa naugua?” aliuliza Lissu akirejea mazungumzo hayo na Suluhu juzi jioni.

“Nilimpa ujumbe huo na napenda kuamini ataufikisha na ujio wake peke yake unatakiwa kufungua milango kwa wale waliokuwa wanafikiri wamefungiwa.”

Alisema suala la Bunge kuwa mbali naye ni mfano mwingine unaotia shaka kuhusu kushambuliwa kwake.

“Mimi ni mbunge na ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, ninatambuliwa na Sheria za Tanzania, Sheria inayohusika ni ya uedeshaji wa Bunge. Sheria inaeleza kwamba mbunge anapoumwa atapata matibabu pamoja na gharama nyingine kutoka bungeni,” alisema.

Lissu alisema kila mbunge anayeumwa analipiwa gharama zote na Bunge na vile vile kama itabidi, alazwe nje ya Dodoma iwe Dar es Salaam, Afrika Kusini, India Marekani au Kenya.

“Analipwa posho na Bunge na mtu anayemuuguza analipwa posho vile vile, nusu ya posho ya mbunge ili kumudu gharama za maisha,” alisema.

“(Lakini) Tangu nimeumizwa, Spika anajua, alitangaza bungeni mbunge mwenzetu anaumwa. Tangu wakati huo mpaka leo Spika hajaja, Katibu wa Bunge, Tume ya Bunge haijaja,” alisema Lissu, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema.

Alisema kuna wabunge wawili CCM, Mary Chatanda (Korogwe Mjini) na Fakharia Shomar Khamis (viti maalum na mmoja wa watumishi wa Bunge walifika siku ya Jumapili, siku ambayo si ya kazi.

“Walikuja kunipa pole, walikaa hapa wakanipa nipa pole, halafu wakaniaga. Nikawauliza mmetumwa chochote, wakasema hapana,” alisema.

“Nikamuuliza ofisa wa Bunge, ‘kuna ujumbe umetumwa uniletee, akasema hapana. Kwa hiyo hao wawili walikuja kibinafsi tu.

“Tume ya Huduma za Bunge inayoshughulikia mambo haya, haijaja mpaka leo. Kwa hiyo ukiachilia mbali matangazo ya Spika, Bunge halijaja kabisa, halijanishughulikia kwa lolote.

“Hakuna anayeomba fadhila, nataka haki, nitendewe haki, anayetendewa mbunge yoyote anayeumwa. Hakuna anayelilia fadhila hapa, hakuna anyeomba ufadhili. Nataka Bunge litimize wajibu wake wa kisheria. Hili nitalipigania, kama siwezi kudai haki yangu ya kisheria ambayo iko wazi, kama ya kwangu naona inakanyangwa kwa makusudi tu, nitapigania ya nani?”

Lissu alisema Bunge halina sababu za maana za kutomgharimia, bali ni kupiga chenga tu.

“Wameandikiwa barua na ndugu yangu mara hawajaiona, kwa hiyo lazima nipiganie haki yangu ili nipiganie haki za wengine,” alisema.



Niliona watu wawili wenye silaha

Katika mahojiano hayo na Mwananchi yaliyochukua takriban dakika 60, Lissu pia alielezea jinsi shambulio dhidi yake lilivyofanyika Septemba 7, lakini tofauti na kauli ya ndugu zake kuwa anawajua watu hao, alisema hawafahamu watu hao na kusisitiza suala la wachunguzi kutoka nje.

“Nilitoka bungeni muda wa saa saba hivi,” alisema.

“Kabla sijatoka nilichangia mjadala wa mkataba kati ya Malawi na Tanzania kuhusu Mto Songwe. Baada ya kumaliza kuzungumza nikakaa kidogo kisha nikatoka na kwenda nyumbani kwa chakula cha mchana.

Alisema alivyofika nyumbani, wakatokea watu eneo la kuegesha magari katika nyumba hizo za Serikali, ambako anaishi jengo moja na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, mbunge wa Ulanga Magharibi (CCM), Dk. Haji Mponda na mmoja wa makatibu wakuu wa wizara.

“Kwa hiyo nakaa katika nyumba za Serikali. Watu wameingia katika nyumba za Serikali zinazolindwa saa 24, block inayotazamana na nyumba yangu, anakaa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson na huwa kuna polisi nje saa 24,” alisema.

“Lakini watu wameingia wenye silaha, wakaja kunishambulia. Sikuwatambua kwa sababu nilishambuliwa nikiwa katika gari sikutoka nje. Dereva wangu aliniambia kuna watu wako nyuma wananifuata nisifungue mlango.”

Alisema alijaribu kuwaangalia kwa kutumia kioo cha pembeni ya gari na kuwaona watu wawili wakitoka na bunduki. Yaliyofuata nimekuja kujikuta nipo hapa nilipo leo wiki moja baadaye.

“Kwa hiyo, siwezi kusema ninawafahamu walionishambulia. Sikutambua hata mmoja wao ila najua nilishambuliwa na watu wawili katika gari iliyokuwa na vioo vyeusi.”

Lissu alisema wiki tatu kabla ya shambulio hilo alilalamika hadharani kwamba anafuatiliwa kila anapokwenda na siku moja aliwasimamisha watu hao katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro na kuwauliza sababu za kufanya hivyo.

“Niliwauliza kwa nini wananifuata na kama kuna mtu kawatuma, mwambieni mimi si mhalifu. Lakini sikupewa ulinzi wowote,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Popular