Viashiria hatarishi vya Elimu vyawatesa watendaji wa Serikali. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 29 November 2017

Viashiria hatarishi vya Elimu vyawatesa watendaji wa Serikali.

 
 Licha ya serikali kufanikiwa kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu nchini lakini inakabiliwa na changamoto ya ufanisi na utendaji wa baadhi ya watendaji ambao wanashindwa kuendana   na mabadiliko yanayotokea katika sekta hiyo.

Ili kuhakikisha watendaji wa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi na kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa usimamiaji na utekelezaji wa miradi ya elimu, wizara hiyo imeamua kuwajengea uwezo watendaji wake.

Hatua hiyo ya wizara itawapa nguvu watendaji katika idara zao kufanya maamuzi sahihi yanayolenga kuinua ubora wa elimu nchini na kuachana na kasumba ya kuwasubiri viongozi wa kitaifa kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amewataka watendaji wa wizara hiyo kubaini changamoto walizonazo katika idara zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu ili kudhibiti viashiria vyote vinavyojitokeza katika utekelezaji wa mipango na malengo ya wizara hiyo.

Prof. Ndalichako ametoa wito huo akiwa Morogoro katika kikao cha kuwajengea uwezo watendaji wa wizara yake ili kuhakikisha sekta ya elimu inaondokana na viashiria hatarishi ambavyo vimekuwa vikijitokeza na kuathiri ubora wa elimu inayotolewa.

Kulingana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) hatua kubwa imepigwa katika kuboresha miundombinu ya shule na watoto wengi wako shuleni lakini changamoto iliyobaki ni ubora wa elimu ambapo elimu inayotolewa haikidhi mahitaji ya soko la ajira. Hii ina maana kuwa wanafunzi hawapati maarifa na ujuzi wa kutosha kuweza kushindana katika soko la ajira na kuibua mbinu mpya za uzalishaji katika nchi husika.

Sababu mojawapo inayokwamisha elimu ni kutokuwa na wataalamu wa elimu waliobobea katika utekelezaji wa majukumu ya kisera. Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimesaini makubaliano ya SDG’s ya kuinua ubora wa elimu na njia mojawapo ni kuwajengea uwezo watendaji wa sekta ya elimu kwa kuwaongezea maarifa na ujuzi yanayoendana na mabadiliko ya kielimu.

Katika kikao hicho watendaji hao watajifunza mbinu mbadala za kukabiliana na viashiria ambavyo vinaonekana kukwamisha utekelezaji wa mipango ya wizara. Lakini lengo kuu la kikao hicho cha pamoja ambacho kinawakutanisha Wakurugenzi Wasaidizi, Waratibu na Wasaidizi wa Miradi, Wadhibiti na Wakuu wa Vitengo vya Wizara ni kuzuia madhara na kuipatia sekta ya elimu mafanikio yaliyokusudiwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza na watendaji wa wizara hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Leonard Akwilapo amesema kikao hicho cha viongozi wa wizara kinalenga kutengeneza mpango mkakati utakaotumika kama muongozo maalumu kukabiliana na viashiria hatarishi.

Amesema mpango huo ukitekelezwa utaleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu na kuwa msingi wa kutatua changamoto zitakazokuwa zinajitokeza katika utekelezaji wa sera ya elimu nchini.

Changamoto inayojitokeza

Kutokana mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayotokea duniani, viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia elimu, wanapaswa kuendana na kasi hiyo kwa kubuni njia mbadala zitakazoongeza ufanisi wa utolewaji wa elimu.  Hatua hiyo itaifanya elimu inayotolewa kwa wanafunzi kuwa na maarifa sahihi ili kushindana katika soko la ajira.

Shirika la Elimu, Sayansi, Utamaduni la Umoja la Mataifa (UNESCO) linaamini kuwa elimu ni haki ya kila mtu na utolewaji wake lazima uendane na ubora.

Ili mikakati ya viashiria hatarishi vya malengo ya elimu nchi wahisani wanahimizwa kutengeneza mifumo imara ya sheria na sera ambazo zinafanya kazi kwa uwazi na uwajibikaji.

Pia kuwa na serikali jumuishi ambayo itawaleta pamoja wadau wa elimu katika ngazi zote za maamuzi na sekta ili kuwa na wigo mpana wa kufanya maamuzi juu ya mustakabali wa elimu.

No comments:

Post a Comment

Popular