Mgombea CCM asakwa na TAKUKURU kwa mahojiano. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 29 November 2017

Mgombea CCM asakwa na TAKUKURU kwa mahojiano.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imetangaza kumsaka mmoja wa wagombea uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kwa mahojiano akituhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Wanachama wa CCM wanaowania uenyekiti katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Desemba 3,2017 ni Msuto Chirangi, Thobias Raya na Samuel Kiboye, maarufu Namba Tatu.

Akizungumza kwa sharti la kutomtaja jina hadi atakapotiwa mbaroni, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Alex Kahunda amesema taasisi hiyo pia inawasaka wanachama wawili wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), wanaodaiwa kuwa mawakala wa mgombea huyo wanaodaiwa kuzunguka kugawa rushwa kwa baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa.

Awali, Kahunda aliwaambia wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa UVCCM unaofanyika mjini Musoma leo Jumatano Novemba 29,2017 kuwa taasisi hiyo inafuatilia nyendo za wote wanaowania uongozi ndani ya CCM na jumuiya zake.

Ameonya kwamba yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa ataishia mikononi mwa maofisa wa TAKUKURU.

No comments:

Post a Comment

Popular