Mke wa Joshua Nassari kumtetea Godbless Lema kwenye kesi ya uchochezi. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 15 November 2017

Mke wa Joshua Nassari kumtetea Godbless Lema kwenye kesi ya uchochezi.

 
MKE wa mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, Anande amejitosa kumtetea mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kwenye shauri la uchochezi analodaiwa kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Anande anachukua mikoba ya wakili wa awali, Sheki Mfinanga aliyeamua kujitoa kumtetea Lema baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa shauri hilo inalosikilizwa na kaimu hakimu Mkazi Mfawidhi, Desder Kamugisha.

Hata hivyo shauri hilo lilishindwa kuendelea jana baada ya hakimu Kamugisha kuwa na kazi nyingine hivyo shauri hilo kiahirishwa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha Jasmin Abdul mpaka desemba 14, mwaka huu.

Mfinanga akijitoa kwenye shauri hilo mbele ya hakimu Kamugisha baada ya kuieleza mahakama namna alivyoomba kupatiwa nakala ya mwenendo wa shauri hilo na uamuzi mdogo mara tatu bila mafanikio ili aweze kwenda mahakama kuu kupinga uamuzi mdogo wa hakimu huyo kugoma kujitoa kwenye shauri hilo.

alisema kuwa baada ya hakimu huyo kukataa kujitoa septemba 25, mwaka huu aliwasilisha mahakamani hapo maombi ya mdomo ya kupatiwa nakala ya uamuzi huo pamoja na mwenendo ambapo aliandika barua ya kukumbushia Oktoba 2, mwaka huu na jana asubuhi lakini hakupatiwa.

Alipinga uamuzi wa Hakimu Kamugisha kuendelea na shauri hilo wakati wao wamewasilisha kusudio la kukata rufaa alilodai kuwa lina hadhi sawa na rufaa huku akimtaka hakimu huyo kurejea uamuzi wake alioutoa nevemba 11, mwaka jana kwenye shauri hilohilo aliodai kuwa haukupingwa na mahakama za juu ila walitaka maombi ya rufaa yawasilishwe kwa wakati muafaka baada ya mahakama kumaliza kutoa uamuzi

Wakili wa Serikali, Khalili Nuda alipinga hoja hizo kwa madai kuwa kusudio la kukata rufaa huwa na hadhi ya rufaa pale linapotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, (DPP) huku akirejea sheria ya uendeshaji mashauri ya jinai iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2008 bila kutaja kifungu cha sheria jambo ambalo wakili Mfinanga alimpinga.

Akitolea uamuzi hoja hizo hakimu Kamugisha alikubaliana na wakili Mfinanga kuwa ni kweli alitoa uamuzi huo novemba 11, mwaka jana lakini haumbani kwa kuwa mahakama hiyo haifanyiwi rejea kwenye maamuzi.

Hata hivyo alikubaliana na hoja wakili wa Serikali, Nuda kuwa notisi ya mdomo ya DPP ndiyo yenye hadhi ya rufaa huku akirejea vifungu vya sheria kuthibitisha hilo hivyo kusema msimamo wake wa awali wa kutaka shauri hilo uendelee uko palepale mpaka watakapopata taarifa rasmi kuwa rufaa imefunguliwa mahakama Kuu.

Alisema kuwa ameona nakala za kuomba mwenendo huo kwenye jalada la kesi hivyo akadai anaamini utawala watampatia wakili wa Lema nakala ya mwenendo huo mapema ili aweze kukata rufaa kwani ni haki yake hivyo akataka kesi iendelee kwa upande wa Jamhuri kuleta mashahidi waliowaandaa.

Wakili wa Lema, Sheki hakuridhika na uamuzi huo hivyo akaileza mahakama, "Nashindwa namna ya kuendelea na kesi hii najitoa kuendelea kumwakilisha lema kwenye hili shauri kwa kile ninachokiona kwenye wigo wa kisheria kutokana yaliyotokea septemba 25 na leo naomba kujiondoa kwenye shauri hili,".

LEMA AMESEMA INAWEZEKANA VITISHO VIMEMUONDOA WAKILI

Lema aliiomba mahakama kumpa muda wa kutosha kumpata wakili anayemuamini huku akidai kunaweza kuwa na mitazamo tofauti juu ya kujitoa kwa wakili wake wakati huu hasa mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu akiwa kitandani kwa kushambuliwa kwa risasi.

Hata hivyo Hakimu Kamugisha alimkatisha asiendelee na hoja hiyo hivyo Lema akaendelea kusisitiza kuwa endapo atakosa wakili anayemuamini atasimama peke yake mahakamani kujitetea.

Aidha Lema alijaribu bila mafanikio kuikumbusha mahakama kuwa hana imani na hakimu huyo ambaye alimkatisha kwa kumweleza kuwa hayo yalishaamuliwa.

Wakili wa Serikali Nuda alisema kuwa walikuwa wameshaandaa shahidi mmoja ambaye alimleta mbele ya mahakama, Inspekta Arstides.

Shauri hilo limeahirishwa mpaka novemba 14, mwaka huu kumwezesha Lema kupata wakili mwingine na upande wa Jamhuri uendelee kwa kuleta mashahidi.

Awali septemba 25, mwaka huu Hakimu huyo aligoma kujitoa kusikiliza kesi hiyo licha ya Lema kumtaka afanye hivyo kwa kile alichodai kuwa aliwahi kufanya maamuzi kwa hila yakampelekea kusota maabusu zaidi ya miezi minne.

Aidha hakimu huyo aliamua kuendekea na shauri hilo hata pale mawakili wa Lema walipowasilisha kwa mdomo kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu kwa lengo la kupinga uamuzi huo mdogo.

Wakili wa Lema, John Mallya aliieleza mahakama kuwa hoja ya mteja wake kuwa hakimu Kamugisha alitoa maamuzi ya hila dhidi yake yanapewa uzito na maamuzi ya mahakama Kuu yaliyotolewa na Jaji Salma Magimbi aliyeweka wazi kuwa mahakama ilishindwa kutumia vizuri mamlaka yake hivyo kukubali kuingiliwa na Kumkataa hakimu Kamugisha kwani

Katika hoja ya pili wakili wa Lema aliieleza mahakama kuwa kuna shauri lingine hakimu huyo aliwahi kumpa haki ya dhamana mteja wake ambapo waliomba ahirisho fupi ili aweze kutekeleza masharti hayo kwa kutafuta wadhamini lakini hakimu huyo hakusema kama amekubali au amekataa ombi hilo badala yake alienda kusaini hati ya kumpeleka rumande.

Hata hivyo alifanikiwa kukidhi masharti ya kabla utekelezaji wa yeye kupelekwa mahabusu haujafanikiwa ingawa alitumia nguvu.

"Ilibidi mteja wetu atumie nguvu kuingia kwenye mahakama yako ili akamilishe masharti yake ya dhamana huku akinyooshewa mtutu wa bunduki na OC CID wa wilaya ya Arusha,Damas Massawe,mteja wetu anatoa rai kwamba haoni kusikiliza kesi hii iliyopo mbele yako kama utaisikiliza kwa haki na usawa," alisema wakili Mallya.

Alisema hakimu huyo ndiyo akifanya maamuzi kwenye kesi mbili za mteja wake ambazo maamuzi yake yamekuwa ya kihistoria hivyo kusisitiza ,"natoa rai kwa heshima mahakama yako wewe ujitoe kusikiliza kesi hii ili Hakimu mwingine apangiwe kesi hii ili aweze kusikiliza bila kuwa na hila,".

Wakili wa Serikali Nuda aliitaka mahakama itupie mbali hoja hizo kwani anaamini hakimu alitoa uamuzi kwa kuzingatia sheria huku akidai kuwa mawakili wa Lema wana nia ya kuchelewesha usikilizwaji wa kesi.

Hakimu Kamugisha akitolea uamuzi mdogo hoja hizo alisema kuwa hazina mashiko hivyo kuzitupankwa kile alichoeleza kuwa jaji au hakimu hawezi kujitoa kwa sababu za kudhania kufikirika au zinazotokana na uoga.

"Mahakimu na majaji japo ni wasomi wa sheria huwa wanafanya makosa ya kisheria ndiyo maana tunasema mtu asiporidhika na uamuzi wa mahakama anakata rufaa ambapo anaweza kuwa na sababu za aina mbili za mantiki au kisheria," alisema hakimu huyo na kuongeza.

"Mshitakiwa anapopewa dhamana anatakiwa akatimiza dhamana na hilo ndilo lililofanyika baada ya kutimiza masharti ya dhamna na lakini baada ya kutimiza masharti alioewa,kwa sababu hizo mbili sioni msingi wa hila,kwa maana hiyo maombi ya mshitakiwa ya kujitoa kwenye kesi hii nimeyakataa na kesi itaendelea mbele yangu,".

Baada ya uamuzi huo wakili Mallya anayemtetea Lema aliieleza mahakama hawajaridhika na uamuzi huo hivyo akawasilisha kusudio la mdomo la kukata rufaa mahakama Kuu.

Hakimu Kamugisha alisema hawezi kuzungumzia uhalali wa maombi hayo hivyo akaagiza shauri hilo kuendelea mahakamani hapo huku wakisubiri mawakili wa Lema wamalize mchakato wa rufaa.

MASHAHIDI TISA NA VIELELEZO VITATU KUWASILISHWA

Mashahidi kwenye shauri hilo ni Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha(OC CID),Damas Massawe, Joseph Labia, W 7006 DC Tausi Hussein na H 2263 PC Musa ambao wote ni askari wa Kituo cha Polisi cha Kati jijini hapa.

Wengine ni Inspekta Aristedes Kasigwa kutoka Francis Bureae, Makao Makuu ya Polisi jijini Dar Es Salaam, Silvester Meda mkazi wa Sanawari, Lilian Joel (Kaloleni), Bakari Juma(Kwa Mrefu),Gofrey Laizer(Baraa).

Wakili Nuda alitaja vielelezo watakavyotumia kwenye shauri hilo kuwa ni pamoja na digital video casset ,(DVC), aina ya Sony, kamera aina ya Sony DVCAM yenye serial namba 7.2 V 222470 na ripoti ya uchunguzi ya kitaalamu ya tape ya video.

Awali Lema anadaiwa Oktoba 23 Mwaka jana katika mkutano wa hadhara viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa, Lema alitoa maneno kuwa; “Kiburi cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu, Mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshamchukua maisha yake.”

“Rais ana kiburi, Rais kila mahali watu wanaonewa,wafanyakazi wa serikali hawana amani, wafanyabiashara hawana amani,watu wananyanyaswa.”Lema alinukuliwa na Wakili wa Serikali, Mtenga.

No comments:

Post a Comment

Popular