Baraza la habari Tanzania ( MCT) kuwachukulia hatua wanao wanyanyasa waandishi wa habari. - KULUNZI FIKRA

Thursday 2 November 2017

Baraza la habari Tanzania ( MCT) kuwachukulia hatua wanao wanyanyasa waandishi wa habari.

 Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesema litawachukulia hatua ikiwamo kuwafikisha mahakamani watu watakaowazuia na kuwanyanyasa waandishi wa habari wakiwa kwenye majukumu yao.

Akizungumza leo Alhamisi wakati wa siku ya kimataifa ya kupinga jinai dhidi ya wanahabari, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga amesema baraza hilo haliridhishwi na hali ya uhuru wa habari iliyopo hivi sasa.

Amesema hatua hiyo inatokana na kukithiri kwa matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya viongozi pamoja na upindishwaji wa sheria unaolenga kuwakandamiza wanahabari.

Amesema kwa kipindi cha miezi sita iliyopita kasi ya kufungiwa kwa magazeti imeongezeka ambapo hadi sasa magazeti sita yamefungiwa huku baadhi ya waandishi wakishambuliwa hali inayozidi kuhatarisha usalama wao.

Ameyataja magazeti hayo kuwa ni gazeti la Mwanahalisi, Mawio, Mseto, Tanzania Daima na Raia Mwema ambayo yalifungiwa kinyume na sheria.

"Waziri hana mamlaka ya kulifungia gazeti lakini isipokuwa kuzuia content (maudhui) fulani ambayo inaonekana kuwa ya kichochezi," amesema

Amewataka waandishi wa habari kuendelea kuripoti matukio ya unyanyasaji ili hatua ziweze kuchukuliwa.

No comments:

Post a Comment

Popular