Freeman Mbowe zaidi kumkomalia kardinali Pengo kwa kauli yake - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 10 October 2017

Freeman Mbowe zaidi kumkomalia kardinali Pengo kwa kauli yake

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameonyesha kusikitishwa na kauli ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyoitoa siku za karibuni kuwa haoni umuhimu wa Katiba, Mbowe anasema kauli hiyo inawasikitisha.

Mbowe ametumia ukurasa wake wa Facebook kufikisha ujumbe wake na kusema kuwa Kardinali Pengo ni kiongozi wa kanisa na watu wengi wanamuheshimu lakini kauli yake hiyo kuhusu Katiba inawafanya wafikiri mara mbili mbili.

"Kardinali Pengo ni kiongozi wa kanisa, anaheshimika na wananchi ambao ni wale anaowaongoza, lakini kauli yake kuhusu Katiba imetushangaza na imetusikitisha. Suala la elimu, chakula na maisha yetu, yanalindwa na Katiba, ndiyo msingi wa mfumo wa rasilimali za Taifa, anaposema haoni umuhimu wa Katiba anatufikirisha, anataka kusema mchakato wa Katiba ulioligharimu Taifa mabilioni ya fedha leo hauna maana?" alihoji Freeman Mbowe.

Aidha Freeman Mbowe alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa umefika wakati mchakato wa Katiba ambao ulikwamba kuendelezwa zaidi ili kuweza kupata Katiba bora
"Umefika wakati mchakato wa Katiba uliokwama ukaendelezwa, na hasa kuanzia katika rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti, Jaji Mstaafu Joseph Warioba. Katiba ni maridhiano, tunahitaji kupata maridhiano ya pande zote, nirudie kwamba alichokisema Kardinali Pengo "kinasikitisha"" alisisitiza Mbowe

No comments:

Post a Comment

Popular