Dar es salaam: Milioni 10 zimeibiwa kwenye makazi ya mapadri - KULUNZI FIKRA

Monday, 30 October 2017

Dar es salaam: Milioni 10 zimeibiwa kwenye makazi ya mapadri

 Watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevamia makazi ya paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohane ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kuiba mali yenye thamani ya zaidi ya Sh10 milioni.

Kabla ya wizi huo, walimfunga kamba paroko na msaidizi wake, pia walimpiga mlinzi aliyekuwa zamu.

Akizungumza na kulunzifikra blog, Paroko Aureus Mwinuka amesema kundi la watu kati ya 15 na 20 walivamia makazi yake usiku wa kuamkia leo Jumatatu Oktoba 30,2017.

“Kundi la watu hao lilifika hapa saa tisa usiku, walikata dirisha na kuingia ndani. Walitufunga kamba mikono na miguu wakitaka tuonyeshe fedha zilipo,” amesema Mwinuka.

Amesema vijana hao walifika nyumbani kwake wakiwa na magari matatu yaliyoegeshwa mbali kidogo na hawakuwa wamefunika sura zao.

“Walikuja na silaha, yakiwemo mapanga lakini hawakutujeruhi. Tukio hilo lilidumu kwa takriban dakika tano kisha wakaondoka,” amesema.

Amesema baada ya wezi hao kuondoka walipiga simu kwa majirani na kwa watu wa kanisa. Pia, taarifa ya uvamizi huo imetolewa katika Kituo cha Polisi Mbezi kwa Yusuph.

Mlinzi aliyekuwa zamu, Simon Chagwa amesema alifungwa kamba na kwamba, kijana mmoja alibaki nje akimlinda wakati wenzake wakiingia ndani. Pia, amesema walimpiga kwa vipande vya tofali.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Malamba Mawili uliopo Kata ya Msigani, Shabani Mgweno amesema amepokea taarifa za tukio hilo na kwamba, alifika eneo la tukio saa 10:00 alfajiri ambako aliwakuta majirani.

Mgweno amesema yamekuwepo matukio ya wizi katika mtaa huo, hivyo ataitisha mkutano wa wananchi ili kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Murilo Jumanne amesema wamepata taarifa na upelelezi unaendelea.

No comments:

Post a Comment

Popular