Zitto kabwe: Huu sio Utanzania ni Umafia - KULUNZI FIKRA

Friday 8 September 2017

Zitto kabwe: Huu sio Utanzania ni Umafia

Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia Chama Cha ACT Wazalendo, Zitto Ruyagwa Kabwe, amesema matukio ya uhalifu yanayoendelea nchini likiwemo tukio la kupigwa na risasi kwa Tundu Lissu yanatisha nchi, na huo sio utanzania wetu.

Kwenye ukurasa wake wa facebook Zitto Kabwe ameandika ujumbe akisema kwamba tukio hilo lililomtokea Tundu Lissu ni ukatili wa hali ya juu na umafia, kitu ambacho siyo matendo yanayotakiwa kufanywa na Watanzania.

"Kilichotokea na kumpata ndugu yetu Lissu jana, ni kitendo cha kihalifu na kisichoendana kabisa na utamaduni wetu wa ustahimilivu na udugu ambao nchi yetu imekuwa ikisimamia, kitendo kile cha kikatili kinakwenda kinyume kabisa na misingi ya utaifa wetu ambao tumekuwa tukiujenga kwa miaka 25 sasa kwa kuwa na taifa huru kidemokrasia, watanzania tunaolitakia mema taifa hili tuna kila sababu ya kulaani na kukataa kabisa utamaduni huu wa kimafia kuzoeleka katika taifa letu, tusimame kulaani kwani huu si Utanzania", aliandika Zitto Kabwe.

Zitto Kabwe aliendelea kwa kusema kuwa pamoja na tofauti ambazo wanakuwa nazo katika baadhi ya mambo na viongozi wengine wa upinzani, lakini imani yake kubwa ni kwamba kwa pamoja wataifikisha Tanzania sehemu nzuri, na kwamba tukio hilo limemfanya akose usingizi.

Tundu Lissu alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya siku ya jana na watu wasiojulikana, na mpaka sasa taarifa zinasema kuwa hali yake inaendela vizuri yupo nchini Kenya kwa matibabu.

No comments:

Post a Comment

Popular