Manji atumia kesi inayomkabili kuelezea hisia zake " mimi bado ni diwani" - KULUNZI FIKRA

Friday 8 September 2017

Manji atumia kesi inayomkabili kuelezea hisia zake " mimi bado ni diwani"

Mfanyabiashara Yusuf Manji Ijumaa hii ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba yeye bado ni Diwani wa Mbagala Kuu na hatambui kuvuliwa udiwani.
Manji alitangazwa kuvuliwa udiwani na Meya wa Temeke, Abdallah Chaulembo September 6/2017.

Manji ametoa malalamiko hayo, kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili na wenzake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Katika kesi hiyo ambayo wakili wa serikali mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi amedai upelelezi haujakamilika, Manji amedai ameona habari kupitia gazeti la Mwananchi kwamba amevuliwa udiwani.

Amedai kama ni kweli amevuliwa Udiwani hatambui, kwani ana miezi 2 yupo gerezani na serikali inatambua kwamba yeye ni Diwani.

“Vikao vya awali vya udiwani wa Halmashauri ya Temeke nilikuwa naudhuria kwa kuwa naheshimu mahakama na kwa uzito wa hii kesi sikutaka kupeleka hata maombi ya dhamana mahakamani,”

“Hivyo mahakama imuagizie DPP na aiambie Halmashauri ya Temeke kwamba wamenikamata na ndio sababu ya kutoudhuria vikao na kama wanataka niudhurie DPP aombe remove order nitolewe gerezani ili niende kwenye vikao,”

Pia Manji amedai kuwa kama hilo haliwezekani, basi wamuandike barua itakayoonyesha agenda ya vikao vyote na yeye atazijibu kwa njia ya barua.

“Ninachotambua mimi ni Diwani wa Mbagala Kuu na kama nimevuliwa au sijavuliwa udiwani sitambui, kwani tayari nimetumia fedha zangu mwenye zaidi ya tsh.Mil 70 na sio za halmashauri kwa ajili maendeleo ya wananchi wangu,”.

Pia amedai kuwa hiyo kesi ni nzito na DPP hapaswi kuangalia upande wake wa kesi tu, kwani yeye amechaguliwa na wananchi na anawasaidia.

Awali kabla ya kuelezwa hayo, wakili wa utetezi Seni Malimi alidai kuwa wanatarajia kuwasilisha maombi ambayo ni ya siri katika tarehe ijayo.

Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Mashauri akautaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanalifanyia kazi suala hilo, ambapo kesi imeahirishwa hadi September 18/2017.

Mbali na Manji, washitakiwa wengine waliokabidhiwa ni Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda, Mtunza stoo, Abdallah Sangey na Thobias Fwere.

No comments:

Post a Comment

Popular