Wanasiasa wamjia juu Omari Mahita - KULUNZI FIKRA

Monday, 11 September 2017

Wanasiasa wamjia juu Omari Mahita

 Siku moja baada ya mkuu wa zamani wa Jeshi la Polisi, Omari Mahita kutoa ushauri wa kukabiliana na changamoto za wanasiasa, vyama vya upinzani vimesema hauna mashiko na unajenga uadui kati ya chombo hicho cha dola na wanasiasa.

Juzi, Mahita alinukuliwa akisema kuwa miongoni mwa mambo waliyomshauri mkuu wa sasa, Simon Sirro ni namna ya kukabiliana na changamoto za wanasiasa.

Mahita alisema kushughulika na wanasiasa ni kazi.

Lakini ushauri huo haujapokelewa vizuri na wanasiasa waliozungumza na gazeti hili, wakirejea matukio yaliyowakabili enzi za uongozi wa Mahita.

Badala yake wamemtaka IGP Sirro kusimamia sheria na Katiba katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Wajibu wa polisi ni kulinda raia na halitakiwi kutumia nguvu nyingi kudhibiti wanasiasa badala ya kushughulikia matukio ya uhalifu yanayojitokeza ambayo yameongezeka na hivi karibuni, Tundu Lissu amepigwa risasi na watu wasiojulikana. Tunataka kuona polisi ikidhibiti matukio hayo na si wanasiasa wanaotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na Katiba,” alisema Samwel Ruhuza aliyewahi kuwa katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi.

Mahita alitoa kauli hiyo juzi baada ya kukamilika mkutano kati ya wakuu wa jeshi hilo wastaafu, makamishna wastaafu na IGP Sirro ambaye yupo madarakani hivi sasa.

Alisema wakati akiwa IGP, Mahita alipachikwa jina “ngunguri” alilolisema kuwajibu CUF waliokuwa wakitumia neno la “ngangari” kuonyesha ushupavu wao kisiasa.

Akirejea kumbukumbu za mstaafu huyo wakati wa utumishi wake, Ruhuza alisema Mahita alitekeleza majukumu yake kwa chuki dhidi ya wanasiasa, kabla na baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo.

Alisema Mahita alikuwa ‘mwanasiasa’ aliyetumikia Jeshi la Polisi. Baada ya kustaafu aligombea ubunge lakini aliangushwa katika kura za maoni ndani ya CCM.

“Kabla ya kuwa IGP alikuwa RPC wa Kilimanjaro na alilipua mabomu katika mkutano wa mgombea urais kwa tiketi ya NCCR Mageuzi mwaka 1995, Augustine Mrema,” alisema.

“Baada ya uchaguzi, akapewa nafasi ya IGP. Uchaguzi wa mwaka 2000 aliibua tuhuma kwa CUF za uhalifu ndiyo akasema kama CUF ni ngangari, basi yeye ni ngunguri. Kwa hiyo ni ushauri wa chuki unaolenga kuipasua nchi.”

Naibu mkurugenzi wa uenezi na habari wa CUF, Mbaralah Maharagande aliungana na Ruhuza akisema kauli ya Mahita imepitwa na wakati. Maharagande alisema Mahita asishauri vyama vya siasa vidhibitiwe, bali ashauri vifutwe kabisa.

Alisema vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi na vinafanya kazi kwa kufuata miongozo ya sheria na kanuni.

Pia, alisema vyama vya siasa vinatakiwa kuikosoa Serikali, kutoa maoni kwa uhuru na kwamba, kama Mahita anakerwa basi aishauri Serikali iuondoe mfumo wa vyama vingi nchini.

“Ashauri vifutwe kabisa vyama vya siasa badala ya kuvidhibiti.”

Maharagande alisema Mahita anakumbukwa na wanachama na wafuasi wa CUF kama IGP aliyekuwa akiminya demokrasia ya vyama vingi.

Katibu mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema kauli ya Mahita ina lengo la kudhoofisha demokrasia. “Anaposema wastaafu wamemshauri IGP kuongeza nguvu katika kukabiliana na wanasiasa ana maana awadhibiti wanasiasa. Huku ni kurudisha nyuma demokrasia ya vyama vingi,” alisema.

Muabhi alisema kazi ya wanasiasa ni pamoja na kukosoa baadhi ya mambo yanayofanywa na Serikali kwa lengo la kuyaboresha.

“Sasa kama Mahita anataka polisi wakabiliane na wanasiasa ana maana anataka tunyamaze, tutakuwa wanasiasa wa namna gani,” alihoji.

Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alisema kauli iliyotolewa na Mahita haikuwa na busara, hivyo IGP Sirro anatakiwa kufuata utaratibu na sheria za nchi.

Alisema Sirro ana uwezo mkubwa wa kazi, hivyo anatakiwa kufuata sheria anapomkamata mtu.

“Hata kama ni mhalifu anatakiwa apelekwe kwenye vyombo vya sheria ili mahakama iweze kutoa uamuzi na si kukabiliana na mwanasiasa,” alisema Waitara.

Katibu wa chama cha DP, Abdul Mluya alisema kauli hiyo inajaribu kuwaziba midomo wanasiasa ili wasishauri na kukosoa.

Alisema licha ya Katiba kutoa haki kwa watu kutoa ushauri na kuikosoa Serikali, wanasiasa wakizungumza wanakamatwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, katibu mkuu wa ADC, Doyo Hassan alisema Sirro akiukubali ushauri wa Mahita, wapinzani watapambana nao.

Alisema kauli ya Mahita ni ya ovyo na ya kupuuzwa, ambayo haifanani na mtu ambaye amewahi kuwa kiongozi wa juu wa jeshi hilo.

“Unapomshauri IGP apambane na wapinzani, maana yake ni kwamba unaamsha ari ya wapinzani waseme tunapambana na dola, kwa hivyo Mahita amekuja kutonesha vidonda vilivyopona,” alisema Doyo Hassan.

No comments:

Post a Comment

Popular