TAARIFA KWA WANANCHI KUPITIA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU HALI YA MHE. TUNDU LISSU ALIYEKO MATIBABUNI NCHINI KENYA.*
Kufuatilia shambulio la kikatili la risasi alilofanyiwa Mhe. Tundu Lissu na dereva wake, Adam Simon siku ya Alhamisi, 7 Septemba 2017, mjini Dodoma na kuhamishiwa katika JIji la Nairobi siku hiyo hiyo usiku kwa ajili ya matibabu na usalama, napenda kutoa taarifa zifuatazo kwa Watanzania wote.
UAMUZI WA KUMLETA NAIROBI BADALA YA DAR ES SALAAM.
Tulilazimika kumsafirisha Mhe. Tundu Lissu kuja Nairobi, Kenya kwa sababu mbili kubwa.
1. Maisha ya Mhe Lissu yalikuwa hatarini sana na palihitajika matibabu maalum na ya haraka sana kutoka kwa Madaktari Bingwa wa kutosha sambamba na vifaa tiba visivyo na shaka yeyote ili kuokoa maisha yake kufuatia kazi kubwa na ya kupongezwa ya awali iliyofanywa na Madaktari wetu kadhaa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
2. Hofu Kuu ya usalama wa Mhe. Lissu na dereva wake ilitanda kote nchini Tanzania baada ya shambulio dhidi ya Uhai wao kushindwa kufanikiwa. Busara ya ki-usalama ilitulazimisha kuwatoa wahanga nje ya mipaka ya nchi hadi hapo usalama wao utakapohakikishwa.
3. Upande wa Uongozi wa Bunge na Serikali ulisisitiza kuwa Mhe. Lissu apelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kama sivyo hawatakuwa tayari kubeba gharama yeyote inayohusiana na matibabu yake. Upande wangu na Wabunge wetu wa UKAWA ulisisitiza Mhe. Lissu apelekwe moja kwa moja Nairobi na kama Bunge na Serikali hawatakuwa tayari kubeba gharama za kuokoa maisha ya Mhe. Lissu, basi sisi na Watanzania wenye mapenzi mema watachangia gharama hizo za kuokoa maisha kitibabu na kiusalama.
HALI YA MHE. TUNDU LISSU
1. Mhe Lissu alifikishwa Nairobi kwa ndege maalum ya kukodi usiku saa 7 na kupokelewa na madaktari Bingwa kutoka Hospitali Kuu ya Nairobi na kukimbizwa moja kwa moja hospitali ambapo kazi kubwa ya kuendelea kuokoa maisha yake ilifanywa usiku kucha na jopo la madaktari wa fani kadhaa wasiopungua kumi.
2. Tangu amefikishwa Nairobi, Mhe Lissu amekuwa akipatiwa matibabu masaa yote mfululizo yakihusisha upasuaji kadhaa na uangalizi muhimu katika chumba maalum cha wagonjwa mahututi (ICU).
3. Kwa mara ya kwanza, Mhe. Lissu aliongea jana jioni na Mkewe Alucia na baadaye na mimi, akisema “ Mwenyeki, I survived to tell the tale…. Please keep up the fight”. Maana yake kwa Kiswahili ni “Mwenyekiti, nimeokoka ili niweze kuelezea mkasa huu ….. tafadhali endeleza mapambano”!
4. Leo Jumapili tena, Mhe. Lissu yuko chumba cha upasuaji akiendelea na upasuaji mwingine.
WAGENI MBALIMBALI WAMTEMBELEA
Wageni mbali mbali mashuhuri kutoka nchini Tanzania, Afrika ya Mashariki na hata Jumuia za kimataifa zimekuwa zikifanya juhudi kubwa kumtembelea Mhe. Lissu.
Hata hivyo, ulinzi umeimarishwa katika eneo anakotibiwa Mhe. Lissu na hairuhusiwi wageni kumwona hadi hapo madaktari wakiridhika kuwa hali yake ya kimatibabu inaruhusu.
DEREVA WAKE: NDUGU SIMON MOHAMED BAKARI
Dereva wa Mhe. Lissu, Simon Mohamed Bakari naye tunaye hapa Nairobi akiendelea kupata huduma za kisaikolojia. Alishuhudia shambulio lile na aliokoka kimiujiza. Anasumbuliwa na msongo mkubwa wa mawazo. Naye hatukuona busara kuendelea kumwacha nchini hadi hapo hali yake ya kiafya na kiusalama itakapohakikishwa.
Ni dhahiri kwa aina ya shambulio lilivyokuwa, wauaji walikusudia kuwauwa wote, Mhe. Lissu na hata Dereva wake.
MKAKATI MAHSUSI DHIDHI YA HAKI, DEMOKRASIA NA USALAMA WA VIONGOZI WA UPINZANI NCHINI TANZANIA
Tanzania si Salama Tena baada ya Uchaguzi Mkuu 2015. Ilianza na mauaji ya Mhe. Alphonce Mawazo Mkoani Geita. Wakakamatwa wanaharakati kadhaa na kuteswa kwa kilichoitwa makosa ya kimtandao. Wakapotezwa Kina Ben Saanane. Wakatekwa Wasanii na kufanyiwa mateso makubwa. Wabunge wanafungwa na kushtakiwa kila siku.
Mali, mashamba na hata Biashara za Viongozi wa Upinzani zinateketezwa au kutaifishwa… sasa tunauwawa kwa risasi mchana kweupe!!! Madhila wanayofanyiwa wapinzani na sasa hata wasio Wapinzani bila kufuata misingi ya kikatiba, kisheria na hata ubinadamu unapoteza Utanzania wetu!!
Hapana!! Inatosha. Tutamuenzi Baba wa Taifa aliyetuasa: “tukiwa waoga tutatawaliwa ma Madikteta!”
Wabunge na Viongozi wa Upinzani ndiyo “Target”. Nawasihi viongozi na wabunge wetu wachukue kila tahadhari. Wanachama nao wawe tayari kulinda na kupigania wajibu wetu, usalama wa viongozi na chama chetu kwa ujasiri. Tusipochukua hatua, kesho atadhurika mwingine!
Tamko na agizo rasmi la Chama litafuata karibuni.
GHARAMA ZA MATIBABU
Mhe. Lissu ameumizwa sana, tena sana. Ni ukweli usiopingika kuwa miujiza ya Mungu ni mikubwa, hata kuweza kumwokoa katika bonde la mauti.
Kutokana na ukweli huu, matibabu yake vilevile ni maalum na yanayohitaki wataalam wengi, vifaa tiba maalum na gharama kubwa. Hadi sasa, zaidi ya Shillingi Millioni 100 zimeshatumika kuokoa maisha ya ndugu yetu Lissu.
Thamani ya Mhe. Lissu, ni kubwa kuliko kiwango chochote cha fedha. Kila njia iliyo halali itatumika kupata fedha za kutosha kumtibu Mhe. Na hatimaye kumrudisha kwenye uwanja wa kudai haki, demokrasia na ustawi kwa wote nchini Tanzania.
Napenda kuwashukuru Watanzania wote kwa namna wanavyoendelea kutusaidia wajibu huu mkubwa kwa maombi na michango mbalimbali ya fedha. Tafadhali tusichoke, tuendelee kuchanga.
Nawashukuru Wabunge wote wa CHADEMA kwa namna walivyobeba gharama za awali. Aidha nawashukuru Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujitoa kwao kuchangia matibabu ya Mhe. Lissu.
Nawaomba wote tuendelee kumwombea Mhe. Lissu. Aidha wote tumsifu na kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa miujiza aliyotenda na atakayotenda katika kutukwepesha na roho za kifo na giza katika kuwahudumia Watanzania.
Freeman Aikaeli Mbowe
MKT CHADEMA TAIFA / KUB
Nairobi, Kenya
10 Septemba 2017
Monday, 11 September 2017
Home
Unlabelled
Freeman Mbowe atoa taarifa rasmi ya afya ya Tundu Lissu.
Freeman Mbowe atoa taarifa rasmi ya afya ya Tundu Lissu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Popular
-
Wakati leo hii Rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta akiapishwa, Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Kikwete ametoa sababu kushin...
-
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), Askofu Dkt Fredrick Shoo amefunguka na kusema kuwa kama taifa linahitaji maendeleo...
-
Mbunge wa Jimbo la Temeke (CUF), Mhe Abdallah Mtolea amefunguka na kuweka wazi kuwa mgogoro uliopo ndani ya Chama chake umekuwa ukiathir...
-
Vat leaching gold processing method is the recently technology that practised in developing nations. In Tanzania vat leaching method w...
-
Serikali imekiri kuwepo kwa changamoto kubwa katika uhitaji wa uzoefu katika nafasi za kazi(work Experience) kwa vijana wa Tanzania. ...
No comments:
Post a Comment