Gwajima: Nawashangaa viongozi wa kiroho kukaa kimya kwa Tukio la Lissu - KULUNZI FIKRA

Monday, 11 September 2017

Gwajima: Nawashangaa viongozi wa kiroho kukaa kimya kwa Tukio la Lissu

 Mchungaji Mchungaji Josephat Gwajima wa kanisa la Ufufuo na Uzima amefunguka na kudai anawashangaa viongozi wa kiroho wanakaa kimya na kuacha masuala ya uhalifu yakiendelea katika nchi bila ya kusema lolote juu ya hilo.

Mchungaji Gwajima amesema hayo akiwa Kanisa kwake Jana Jumapili ambapo aliahidi kumfanyia ibada maalum ya kumuombea mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu baada ya kupigwa risasi na watu wasiofahamika akiwa nyumbani kwake Dodoma siku za hivi karibuni.

"Naona huruma sana kwa watu wanaofanya uhalifu katika nchi kwa sababu unapomwaga damu ya mtu na wewe yako itamwaga na mwingine bila ya kujarisha umemwaga kwa sababu zipi. Damu imekuwa ikimwagika sana katika nchi hii kuanzia kule Kibiti. Nashangaa sijui imekuwaje viongozi wa kiroho walikuwa kimya, mimi sikuwepo. Viongozi wa kiroho ni lazima waseme", amesema Gwajima.

Aidha, Mchungaji Gwajima katika maombi yake amewataka watu wanaofanya vitendo vya uhalifu nchini wafanye hima kutubu dhambi zao juu ya wanachokifanya na endapo hawatafanya hivyo basi watambue yatawafika yale yale ambayo walikuwa wakiwatendea wenzao.

"Mambo ya kiuhalifu tunatakiwa kuyakemea bila ya kuwa na uoga wa aina yeyote wala kuangalia upande wowote ule na hivyo ndivyo Mungu anavyotaka, unasema unachotakiwa kusema kama hiki hakipo sawa. Tundu Lissu ana baba, mama, watoto pamoja na mke anatakiwa kuishi", amesisitiza Gwajima.

Kwa upande mwingine, Gwajima amesema hakuna jambo baya kama kuwepo katika nchi halafu hutambui inaeleka wapi.

No comments:

Post a Comment

Popular