Rushwa ndani ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) imemfanya Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni, Prosper Msellem, ajiuzulu.
Pamoja na uenyekiti wa Bodi ya Zabuni, Msellem ni Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti REA.
Kwa msimamo wa kufichua ufisadi, sasa ametakiwa aandike barua ya kujitetea kwanini asifukuzwe huo ukurugenzi.
Hatua hiyo imekuja wiki kadhaa tangu ziibuliwe tuhuma za rushwa na upendeleo kwenye Awamu ya Tatu ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini, unaolenga kufikisha nishati hiyo katika vijiji 3,559 vilivyo kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara. Thamani ya mradi huu ni karibu Sh trilioni moja ambazo asilimia zaidi ya 95 zinatolewa na walipa kodi Watanzania.
Msellem aliteuliwa Januari 13, mwaka huu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni REA. Kwa mujibu wa sheria, uteuzi wa nafasi hiyo hufanywa na Mkurugenzi Mkuu wa REA ambaye kwa sasa ni Injinia Gissima Nyamo-Hanga.
Katika barua ya kujizulu, ametoa maelezo marefu ya kurasa saba, akiibua ufisadi uliofanywa na Bodi ya Wakurugenzi ya REA, na Menejimenti ya REA kwenye mchakato wa ununuzi wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu.
“Najiuzulu ili kutoa nafasi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuweza kufanya kazi zake za uchunguzi kwa uhuru,” amesema kwenye barua yake aliyomwandikia Injinia Nyamo-Hanga.
Nakala ya barua hiyo aliipeleka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini nayo imeguswa na Msellem akisema ilishiriki kuweka shinikizo kwa baadhi ya mambo ambayo ni kinyume cha sheria.
Anasema taratibu za ununuzi kwenye mradi huo ziligubikwa na ukiukwaji mkubwa wa Sheria za Ununuzi wa Umma, akisema bayana kuwa rushwa ilitamalaki.
Anasema kuwa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) pamoja na Menejimenti ya REA zilikuwa zikifanya kazi ya kutekeleza mchakato kwa shinikizo kubwa kutoka kwenye Kamati hiyo.
“REB na Menejimenti zilikuwa zinafanya kazi kwa kupuuza Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni zake za mwaka 2013 na bila kuzingatia uwezo wa ndani wa REA kutekeleza kazi za ununuzi wa mradi huo wa REA Awamu ya Tatu,” amesema Msellem.
Hoja yake nyingine ni kuwa baada ya REB na Menejimenti ya REA kusaini mkataba wa makubaliano ya kutekeleza hatua za ununuzi, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kitengo cha Ununuzi (PMU) cha REA, Kamati za Uchambuzi na Bodi ya Zabuni REA walilazimishwa kufanya kazi katika mazingira magumu.
Anasema hatua hiyo ilisababisha kuwapo vitendo vya ukiukwaji mkubwa Sheria na Kanuni za Ununuzi.
Msellem anatoboa kwamba kulikuwa na tofauti kubwa ya bei zilizopitishwa na Bodi ya Zabuni na bei zilizofikiwa baada ya makubaliano ya zabuni.
Msellem anatoa mfano wa mtumishi mwandamizi wa REA alivyoomba rushwa kutoka kwa mmoja wa wazabuni kwenye Mradi wa Awamu ya Tatu.
Mengine aliyoyafichua kiongozi huyo ni kuwapo wa udanganyifu mkubwa wa makandarasi wenye madaraja yasiyokidhi vigezo lakini walipewa kazi kinyume cha sheria. Anasema baadhi ya makandarasi, ama hawakuwa na vyeti stahiki, walighushi au kampuni hazikuwapo kabisa, lakini waliweza kupenyezwa hadi kwenye hatua ya kusudio la kupewa zabuni.
Sehemu nyingine iliyozungumzwa na Msellem, ni ile inayohusu malipo kutokana na viwango vilivyokadiriwa na makandarasi kwa kazi walizoomba, na kiwango kilichokubaliwa na Bodi.
Anatolea mfano hai wa ‘lot’ zilizo kwenye zabuni namba 9 ambako viwango vilivyoidhinishwa na Bodi vilikiukwa kwa namna ambayo iliashiria rushwa.
Mathalani, kwenye lot Na. 1 iliyohusu mradi wa umeme wilaya za Chato, Nyang’wale, Bukombe na Mbogwe mkoani Geita, kampuni ya Al-Hatimy Developers Limited, kiwango cha malipo kilichopitishwa na Bodi ya Zabuni REA kilikuwa Sh bilioni 56.981; lakini kilichokusudiwa kumlipa mzabuni huyo ni Sh bilioni 59.816. Hilo ni ongezeko la Sh bilioni 2.834.
Lot Na. 2 ilikuwa kwa kampuni za Radi Services Ltd, Njarita Contractor Ltd na Agwila Contractor Ltd. Kampuni hizo za ubia zilipewa kazi katika wilaya za Nanyumbu, Masasi, Newala, Tandahimba na Mtwara mkoani Mtwara. Kiwango cha malipo kilichokubaliwa kwenye Bodi ni Sh bilioni 29.6; lakini kwenye malipo yakawa yameandaliwa malipo ya Sh bilioni 34.083; ikiwa ni ziada ya malipo ya Sh bilioni 4.483.
Kampuni ya Nakuroi Investment ilikuwa imepewa kazi katika wilaya za Kalambo, Sumbawanga na Nkasi mkoani Rukwa. Kiwango cha malipo kilichoafikiwa na Bodi ni Sh bilioni 31.645 lakini kwenye malipo yaliyopangwa kufanywa kiango hicho kilikuwa Sh bilioni 34.662; kikiwa kimezidi kwa Sh bilioni 3.017 ya kile kichoidhinishwa na Bodi.
Kampuni ya Sengerema Engineering Group Ltd, Bodi iliidhinishia malipo ya Sh bilioni 22.238 lakini mwishowe kwenye hatua za malipo kiasi hicho kiliongezwa hadi Sh bilioi 27.031. Hilo ni ongezeko la Sh bilioni 4.792. Kampuni hiyo ilishinda zabuni ya kusambaza umeme katika wilaya za Kibaha, Bagamoyo, Mafia, Rufiji, Kisarawe na Mkuranga mkoani Pwani.
Pia, kampuni ya Steg International iliyokuwa imekubaliwa na Bodi ilipwe Sh bilioni 25.653; ikawa imeandaliwa malipo ya Sh bilioni 29. 916 ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 4.263.
NYAMO-HANGA AMJIBU MSELLEM
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Nyamo-Hanga, amemjibu Msellem kwa hisia kali akisema Mwenyekiti huyo wa Bodi alikuwa na nafasi kubwa ya kuusimamia mchakato wa ununuzi wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu kwa kushirikiana na wajumbe wenzake wa Bodi ya Zabuni REA ili usiende vibaya.
“Na kama haya anayoyasema ni kweli maana yake ni kwamba alijua mambo hayaendi inavyotakiwa na bado akanyamaza akisubiri yaharibike zaidi na baada ya hapo yeye ajiuzulu.
“Kitendo hicho ni cha kinafiki na kinaonesha ukosefu wa uzalendo na kinacholenga kulitia Taifa na wananchi wake hasara kubwa na ni kitendo kinachomkosesha sifa muhimu za kuwa kiongozi.
“Hata hivyo, ukweli ni kwamba taratibu zote za manunuzi zilifuatwa na muda wa kutosha ulitolewa kwa ‘evaluation committee’ na Bodi ya Zabuni kufanya maamuzi yake kwenye hatua mbalimbali za mchakato wa ununuzi wa mradi wa REA Awamu ya Tatu ambayo ni kutaarifu Menejimenti ya REA iliwahi kuiwasilisha kwenye Bodi ya Nishati Vijijini kuhusiana na namna mchakato wa ununuzi wa mradi huu ulivyoendeshwa.
“Ndugu Msellem alikuwa sehemu ya wakurugenzi wa REA walioandaa na kuwasilisha taarifa hiyo kwenye Bodi ya Nishati Vijijini kwenye kikao chake cha dharura cha Aprili 27, 2017 kwenye Ukumbi wa Bodi wa REA na hakuonesha wala kusema kama mchakato huo ulikuwa na dosari.
“Ndugu Prosper Msellem pia kama mjumbe wa ‘Senior Management ya REA’ muda wote alikuwa na nafasi ya kushauriana na wakurugenzi wenzake na hatimaye kumshauri Mkurugenzi Mkuu juu ya jambo lolote ambalo linaelekea kuleta madhara kwa taasisi yetu ikiwamo suala zima la mchakato wa ununuzi wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu.
“Kutofanya hivyo hali akijua kuwa kuna matatizo kama alivyoandika kwenye taarifa yake ya kujiuzulu, kunamfanya kukosa sifa za kukaa kwenye Senior Management ya REA kama Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti,” anasema Nyamo-Hanga.
Pia anasema Msellem, kama mmoja wa wakurugenzi, hakuwahi hata mara moja kuieleza Bodi ya REA upungufu aliouainisha kwenye barua yake ya kujizulu.
“Ndugu Prosper Msellem alipata mamlaka ya kushirikisha mamlaka ya nje kuhusu taarifa yake ya kujiuzulu, angeweza kutumia mamlaka hayo kama Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni REA kuiandikia Bodi ya Nishati Vijijini kuijulisha kuhusu dosari zozote alizokuwa ameziona kwenye mchakato huu wa ununuzi. Kitendo cha kutoishirikisha Bodi ya Nishati Vijijini na badala yake kuchagua kuishirikisha mamlaka nyingine kinaonesha pia kuwa hana imani na Bodi ya REA. Hii pia ni ‘insubordination’ kwa mamlaka iliyomteua kushika wadhifa wa Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti ndani ya REA,” anasema.
Injinia Nyamo-Hanga anaitetea Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kwa kusema: “Kitendo cha kuandika kwenye taarifa yake (Msellem) kuwa ‘Bodi ya Nishati Vijijini kusaini mkataba wa kutekeleza mchakato wa ununuzi wa mradi wa REA Awamu ya Tatu kinaashiria ukosefu mkubwa wa nidhamu kwenye mamlaka hizo na hivyo kumwondolea kabisa sifa ya kuwa mtumishi wa Serikali.”
Anasema Msellem alikuwa akihudhuria vikao vya Kamati hiyo ya Bunge na alishirikiana na wakurugenzi na maofisa wa REA kuandaa mkataba huo, na kwamba hakushauri lolote iwapo Bodi ya Nishati Vijijini, Menejimenti ya REA na Wizara ya Nishati na Madini na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini zilikuwa zinafanya makosa kwa kufanya hivyo.
“Badala yake alikaa kimya mpaka alipoweka tuhuma hizi kwenye barua yake ya kujiuzulu…Kitendo hiki kinaashiria kwa uwazi kuwa mtumishi huyu (Msellem) hana ushirikiano na wenzake katika kutekeleza majukumu ya REA na ya Serikali kwa ujumla na kwamba hayuko tayari kutumia elimu yake, weledi wake, utashi wake na utaalamu wake katika kusaidia mafanikio ya REA kama taasisi na Serikali kwa jumla.
“Taarifa hiyo ya kujiuzulu uenyekiti na ujumbe wa Bodi ya Zabuni ya REA ya Ndugu Msellem haikuzingatia maelekezo ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 ambayo inamtaka mjumbe wa Bodi ya Zabuni anayejizulu kutoa notisi ya mwezi mmoja kwa mkuu wa taasisi kabla ya kufanya hivyo,” anasema na kuhitimisha kuwa:
“Kutokana na taarifa hii ya kujiuzulu aliyowasilisha Ndugu Prosper Msellem ambayo pia inabeba tuhuma dhidi ya Bodi ya Nishati Vijijini, Menejimenti ya REA, Wizara ya Nishati na Madini (ambayo ndiyo msemaji kwenye vikao vya Kamati za Bunge ambayo REA hualikwa) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, mimi Mkurugenzi Mkuu wa REA ninaona kuwa Ndugu Prosper Msellem ni mnafiki na:
“Amepoteza sifa za kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni ya REA;
“Amepoteza sifa za kuendelea kuwa kwenye ‘Senior Management ya REA’ na kumshauri Mkurugenzi Mkuu wa REA;
“Amepoteza sifa za kuendelea kuwa Mkurugenzi katika nafasi yake ya sasa ya kuwa Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti ndani ya REA;
“Amepoteza sifa za kuwa kiongozi katika taasisi yoyote ile ya Serikali;
“Amepoteza sifa na uaminifu katika kushirikiana na wakurugenzi wa REA, Bodi ya Nishati Vijijini, wafanyakazi wengine wa REA katika kutekeleza majukumu ya taasisi hii na Serikali kwa ujumla.”
Taarifa hiyo ya Injinia Nyamo-Hanga ameiwasilisha kwenye Bodi ya Nishati Vijijini.
Wakati Msellem akibanwa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk. Juliana Palangyo, amewaambia wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini kuwa wizara ina taarifa za rushwa zinazowakabili watendaji ndani ya REA na Bodi ya Zabuni.
Amesema karibu watumishi waandamizi wa REA wote wanahusishwa na vitendo vya rushwa, isipokuwa Mwenyekiti aliyejiuzulu, Msellem.
Thursday, 21 September 2017
Home
Unlabelled
Rushwa yaifumua REA: Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni atoboa siri, ajiuzulu
Rushwa yaifumua REA: Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni atoboa siri, ajiuzulu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Popular
-
THIS ANNOUNCEMENT CONTAINS INSIDE INFORMATION Acacia Mining plc (“Acacia” or the “Company” or the “Group”) Management Changes Ac...
-
Tanzania’s Tunduru district is a major producer of gem-quality sapphire and ruby, along with exotic gems such as alexandrite and tsavor...
-
Moto mkubwa umelipuka na kuunguza soko la wafanyabiashara wadogo wadogo (machinga) katika eneo la Mbagala Rangi Tatu – Dar, asubuhi hii M...
-
Ofisi ya Spika wa Bunge imesema, mpaka sasa haijapokea barua toka kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia Chama cha...
-
Spika wa zamani, Pius Msekwa amesema Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu hakuwa analazimika kuandika barua kwa Spika wa Bunge...

No comments:
Post a Comment