Naibu Waziri Jafo: Neema Huduma ya afya yaja - KULUNZI FIKRA

Friday, 15 September 2017

Naibu Waziri Jafo: Neema Huduma ya afya yaja

 
 SERIKALI imetoa agizo la kujengwa na kukarabatiwa kwa vituo 172 vya afya kote nchini na kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha kazi hiyo iwe imekamilika Desemba 30, mwaka huu, na baada ya hapo serikali itaweka vifaa na hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, alisema fedha zinazotakiwa kufanya kazi hiyo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kuhakikisha kwamba linapunguza vifo vya mama na watoto, zimeshafikishwa kunakotakiwa. Jafo alisema kila kituo kimetengewa Sh milioni 500, na kwamba serikali imeshapata na kusambaza Dola za Marekani milioni 66 zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na fedha hizo zitatumika kukarabati vituo vya afya 103.

Alisema Tamisemi imepata msaada kutoka Ubalozi wa Canada wa Dola za Marekani milioni 22 ambazo vituo 44 vitakarabatiwa. Alisema vituo 25 vilivyobaki vitafanyiwa ukarabati kwa fedha za Benki ya Dunia na Mfuko wa Afya wa Pamoja kwa fedha zilizovuka mwaka kwa mwaka 2016/2017. Vituo hivyo 25 vimefikishiwa Sh bilioni 12.5. Fedha hizo zote za ukarabati ni takriban Sh trilioni 8.6. Jafo alisema baada ya kukarabati, serikali itaweka vifaa katika vituo hivyo.

Aliwaagiza wakuu wa mikoa, makatibu tawala, wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri kuhakikisha fedha zilizotengwa zinafanya kazi iliyokusudiwa na kila tarehe 5 ya mwezi unaofuata wafikishe taarifa Tamisemi kwa tathmini. Akizungumzia kwamba kutakuwepo na ufuatiliaji wa karibu wa thamani ya kazi, alisema kipaumbele ni ukarabati na ujenzi wa jengo la upasuaji, ukarabati na ujenzi wa wodi ya kina mama na watoto, ukarabati na ujenzi wa jingo la maabara, nyumba ya mtumishi na maeneo mengine ya kipaumbele kutokana na rasilimali fedha iliyopo kama ilivyoainisha katika waraka ambao tayari umefikishwa kwao kupitia makatibu tawala wa mikoa yote.

Naibu Waziri alisema Tamisemi ndiyo yenye jukumu la utekelezaji wa Sera ya Afya nchini amewataka wakuu wa mikoa, wilaya kuhakikisha kwamba ukarabati huo unaendana na thamani halisi ya fedha; huku akiwataka watendaji hao wa serikali kuhamasisha wananchi kujitolea nguvu kazi katika maeneo yao. Katika utaratibu huo halmashauri itaajiri mafundi, mhandisi wa halmashauri na wataalamu wake watasimamia na hivyo gharama kupunguka na miradi kukamilika kwa wakati.

“Waheshimiwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wahakikishe wanasimamia kikamilifu ujenzi huo ili ukamilike kwa kipindi cha miezi mitatu hadi ifikapo Desemba 30, 2017,” alisema Jafo na kuwataka wawakilishi wa wananchi wabunge na madiwani kufanikisha kazi hiyo. Wakati serikali ikichukua hatua hiyo ya kukarabati vituo vya afya, upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na hospitalini umeimarika kwa kiasi kikubwa kwani kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 81.

No comments:

Post a Comment

Popular