Niyonzima awataka mashabiki kutowalinganisha na Yanga - KULUNZI FIKRA

Friday, 15 September 2017

Niyonzima awataka mashabiki kutowalinganisha na Yanga

 
 Mchezaji wa timu ya Simba na raia wa Rwanda, Haruna Niyonzima amesema, licha ya kulingana kwa pointi katika Ligi kuu ya Tanzania Bara inayoendelea, timu yao na mahasimu wao timu ya Yanga haziko sawa katika kupima uwezo.

Niyonzima, amesema hayo wakati kikosi chao kikilingana pointi na Yanga, wote wakiwa na pointi nne baada ya michezo miwili ya ligi huku Simba ikiwa juu ya Yanga kutokana na idadi kubwa ya mabao waliyonayo.

Timu hiyo ya Simba inatarajiwa kuendeleza dozi zake keshokutwa Jumapili itakapomenyana na Mwadui FC ya Shinyanga, mechi ambayo inatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. 

Mnyarwanda huyo amesema kuwa ni mapema mno kuanza kuwalinganisha uwezo wao na mahasimu wao hao lakini ukweli wa kila kitu utajulikana baada ya kupita kwa michezo tano katika ligi hiyo.

“Yanga ni timu nzuri na kila mmoja analijua hilo kwani wamesajili wachezaji ambao wamewaongezea kitu ndani yao na nilishasema tangu zamani kuwa ni timu nzuri na bora, lakini suala la kuanza kutulinganisha nao nadhani hilo kwa sasa mashabiki wanatakiwa waliweke kando."

“Nadhani itakuwa vizuri kama tutaanza kulinganishwa na timu zote za ligi kuu baada ya michezo mitano ijayo, ambapo michezo hiyo ndiyo itaamua ni nani yuko vizuri kuliko mwenzake na hapo ndipo itakuwa kipimo bora zaidi kwetu na kwao kuliko ilivyo hivi sasa,” alisema Niyonzima.

No comments:

Post a Comment

Popular