Mahita:Tumemshauri IGP Sirro apambane na wanasiasa - KULUNZI FIKRA

Saturday, 9 September 2017

Mahita:Tumemshauri IGP Sirro apambane na wanasiasa



 
 Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu Omari Mahita amesema kuwa miongoni mwa mambo ambayo wamemshauri IGP Simon Sirro ni kukabiliana na wanasiasa.

Mahita amesema hayo Mara baada ya kukamilika mkutano kati ya wakuu wa Jeshi hilo wastaafu na makamishna wastaafu na Mkuu wa Jeshi hilo wa sasa IGP Sirro.

Amesema wamewakumbusha mambo mengi, wamewapa uzoefu wa vitu vingi, lakini kubwa na ambalo ni changamoto ni namna ya kukabiliana na wanasiasa."Kwa mkakati huu tutafika" amesema Mahita.

Mahita amefafanua ukiwa ndani ni ngumu kuona unachofanya, lakini walio nje wanaona na ndiyo maana wamekutana ili kubaini wanapatia wapi na kukosea wapi.

Kwa upande wa IGP Sirro amesema hicho kilikuwa kikao cha kawaida cha kukumbushana wajibu wa kazi zao huku suala la weledi katika utendaji na mafunzo maalumu likijadiliwa kwa kina.

Amesema wastaafu hao wamesisitiza kuona upungufu katika utendaji wa baadhi ya askari wa Jeshi hilo na kuwataka wazingatie weledi.

"Wamesisitiza mafunzo ya mara kwa mara, hususani mafunzo maalumu kama ya uhalifu wa mtandao ambalo limesisitizwa sana ili kuhakikisha Jeshi la Polisi linakwenda na wakati" amesema Sirro.

Naye Mkuu wa Jeshi hilo mstaafu aliyemuachia wadhifa huo Sirro Ernest Mangu alisema ili ujione lazima ujiangalie kwenye kioo, na wao kwa sababu walihudumu kwenye Jeshi hilo ndiyo kioo cha kukosoa, kuboresha na kupongeza.

Amesema kwenye mkutano huo wamejadili mambo mbalimbali ikiwamo ya kiutendaji.

"Naamini wamesikia na watajirekebisha, kwa sababu sisi tulio nje ndiyo tunaona na kusikia yanayosemwa, lengo likiwa ni kuhakikisha Jeshi la Polisi linafanya yanayotarajiwa na jamii" amesema Mangu.

Akizungumza baada ya mkutano huo mkuu wa Jeshi hilo mstaafu Said Mwema amesema wametumia fursa hiyo kujadili mbinu na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu.

No comments:

Post a Comment

Popular