Maalim Seif: Hili la Lissu halijawahi kutokea - KULUNZI FIKRA

Friday, 8 September 2017

Maalim Seif: Hili la Lissu halijawahi kutokea

 
 Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema amesikitishwa na kushambuliwa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu tukio alilosema halijawahi kutokea nchini.

Amesema anampa pole Lissu na kumwombea kwa Mungu amjalie afya na kupona haraka ili aendelee na kazi yake ya kuwatetea wananchi.

Pia, kutetea haki na utawala wa sheria na kupambana na dhuluma, uonevu na hasa dhidi ya wanyonge.

"Tukio hili ni la kusikitisha, ni ushahidi mwingine unaoonyesha nchi yetu inaelekea kubaya. Hali hii inapaswa kudhibitiwa,” amesema.

Maalim Seif amesema leo Ijumaa kuwa, “Bila hatua madhubuti kuchukuliwa za kuiepusha nchi na chuki na kulipizana visasi miongoni mwa wananchi, mambo hayo husababisha machafuko."

Katibu Mkuu huyo wa CUF aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema pamoja na kauli za Serikali kuwa inawasaka wahalifu, anaisihi itumie uwezo wake wote kuwatia mikononi watu waliohusika katika kipindi kifupi kijacho ili wananchi waimarishe imani yao kwa Serikali.

Amesema kuna haja ya uongozi wa Tanzania kuandaa na kuitisha mkutano wa mashauriano ya kitaifa ili kushauriana namna ya kuzuia mgawanyiko nchini.

"Nampa pole Lissu na familia yake, uongozi wa Chadema na wananchi wa Singida Mashariki, pia wananchi wote walioguswa na shambulio hili la kikatili," amesema Maalim Seif.

Lissu aliyeshambuliwa kwa kupigwa risasi tano, mbili kwenye miguu, mbili tumboni na moja mkononi anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan mjini Nairobi, Kenya alikopelekwa jana Alhamisi.

No comments:

Post a Comment

Popular