Katibu mkuu wa wizara ya afya ni mmoja wa madaktari wanaomfanyia upasuaji Tundu Lissu - KULUNZI FIKRA

Thursday 7 September 2017

Katibu mkuu wa wizara ya afya ni mmoja wa madaktari wanaomfanyia upasuaji Tundu Lissu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya ambaye ni mtaalamu wa dawa za usingizi ni miongoni mwa wataalamu wanaoendelea kumtibu mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyejeruhiwa kwa kupigwa risasi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Dk Ulisubisya na wataalamu wengine wanaendelea na hatua ya pili ya upasuaji baada ya ile ya kwanza kufanyika kikamilifu na kwa mafanikio.

Mwalimu amesema walichofanya madaktari katika kazi ya kwanza ni kuhakikisha afya yake inatengemaa kwa kudhibiti damu kuendelea kuvuja.

Waziri Mwalimu amesema baada ya kukamilika kwa hatua hiyo madaktari wataweza kushauri kupitia ripoti iwapo ahamishiwe Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Amesema madaktari wana uwezo kwa kufanya matibabu kwa mbunge huyo na amemhakikishia Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwa wamedhamiria kuokoa maisha ya Lissu ili arejee katika hali yake ya kawaida na kuendelea na shughuli zake za kila siku.

Spika Ndugai amesema taarifa za tukio hilo amezipata akiwa njiani akirejea mjini Dodoma na kwamba, zimewashtua.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za tukio hilo na analaani shambulio hilo.

Amesema shambulio hilo liwe limefanyika kwa sababu za ama kisiasa, hujuma, ujambazi au ugomvi watapambana kwa nguvu zote kuhakikisha waliohusika wanapatikana.

Mwigulu amesema baada ya tukio hilo leo mchana, aliagiza polisi kuweka vizuizi katika njia zote zinazotoka na kuingia Dodoma ili kuhakikisha waliofanya tukio hilo hawapati mwanya wa kutoroka.

“Tunalaani tukio hili ambalo halikubaliki, tutawasaka kuhakikisha tunawakamata wahusika na sheria kufuata mkondo wake. Kubwa, Watanzania tumuombee apate afya njema na aweze kurejea katika shughuli zake za kawaida,” amesema.

Mwigulu amesema kwa shambulio hilo ni Mungu tu amemsaidia hadi hatua aliyofikia sasa. Amewaomba Watanzania kila mmoja kwa dini yake wamuombee Lissu afya yake itengemae.

No comments:

Post a Comment

Popular