Walio bomolewa nyumba zao Kimara wanalala kwenye vifusi wakichochea moto usiku kucha - KULUNZI FIKRA

Monday 28 August 2017

Walio bomolewa nyumba zao Kimara wanalala kwenye vifusi wakichochea moto usiku kucha

 Inasikitisha! Neno hili linatosha kueleza hali halisi ya wakazi wa Kimara Stop Over hadi Kibamba CCM ambao wanalala nje baada ya nyumba zao kukumbwa na bomoabomoa.

Kazi hiyo inatekelezwa na Wakala wa Barabara (Tanroads) kuondoa majengo yaliyo katika hifadhi ya Barabara ya Morogoro, mita 121.5 kutoka katikati ya barabara kila upande kuanzia Kimara hadi Kiluvya.

Waandishi wetu walitembelea maeneo yaliyoathiriwa juzi usiku na kukuta baadhi ya wananchi wakiwa wamelala nje wengi wao wakiwamo watoto, wazee na kina mama.

Walikuwa wamelala kwenye magofu ya nyumba zao, gizani na hatari zaidi ni kwamba sehemu za kujisaidia pia zimebomolewa. Kutokana na hali hiyo, wapo waliotenga maeneo na kuyafanya kuwa vyoo na kutumia moto kupata mwanga na joto kutokana na baridi.

Maisha ‘mpya’
Ziara ya usiku ya waandishi wetu ilianzia Kimara Stop Over ambako waliwakuta waathirika zaidi ya 20 wakiishi kwenye vifusi vya zilizokuwa nyumba zao na mmoja alikuwa ameweka hema.

Waandishi wetu walipofika katika hema hilo, saa mbili usiku juzi, waliwakuta watu wapatao 20 wakiwa wamekusanyika katika hema huku Salma Msisi (50) akisonga ugali pembeni kidogo.

Katika hema hilo, kina baba na kina mama aliokuwa wakiota moto uliowashwa kwa kutumia kuni ambazo ni masalia ya mbao zilizokuwa katika nyumba zao pia kulikuwa na watoto watano wanaokadiriwa kuwa na miaka kati ya mitano hadi minane waliokuwa wamesinzia kwenye mikeka na magodoro.

Kutokana na giza lililokuwapo, ujio wa waandishi uliwastua baadhi yao, “Hao ni kina nani?” alihoji mmoja wao. “Sisi ni watu wema, msiwe na wasiwasi,” alijibu mmoja wa waandishi kisha ‘mwenyeji’ kuendelea, “Haya ndiyo maisha yetu, msishangae, karibuni tuote moto.”

Wakati wote wa makaribisho hayo, Mzee Nicomed Leo (61), ambaye nyumba zake nne zilizokuwa eneo moja, mbili zikiwa za ghorofa moja na nyingine za kawaida zote zimebomolewa, alikuwa ‘bize’ akichochea kuni ziwake vizuri.
Baadaye mzee huyo ambaye aliwahi kuwaeleza waandishi wetu kuwa nyumba zake zilikuwa na thamani ya Sh900 milioni alisema, “hapa ndipo maskani kwetu, tunalala hapa hadi asubuhi.”

Baada ya kusema hayo alicheka kisha akaketi baada ya moto kukolea.
Awali, alipohojiwa na gazeti hili kabla ya nyumba zake kubomolewa alisema amejiandaa kisaikolojia na kwamba atajenga kibanda juu ya magofu na ataishi hapo hadi atakapokufa kwa kuwa aliwekeza ujana wake wote katika eneo hilo lakini siku nyumba zake zilipobomolewa alizimia. Baada ya ugali kuiva, walijigawa makundi mawili na kula kwa pamoja. Uliliwa kwa dagaa.

“Waandishi karibuni tule, mmefika wakati muafaka. Jamani sogeeni huku tupate chakula wapendwa. Waamsheni hao watoto wale kwanza,” hizo ndizo kauli za wakazi hao ambao mazingira yamewalazimu kuishi pamoja. Katika maisha yao mapya, wakazi hao huchangishana kati ya Sh1,000 na Sh500 kulingana na uwezo wa mtu ili kununua chakula. Wengi wao walisema wameuza mbao, matofali na mabati ili wapate fedha za kujikimu kwa wakati huu.

“Nimeuza mbao na matofali kwa bei ya hasara walau nipate fedha za kunisukuma katika kipindi hiki,” alisema Hamis Juma. Kuhusu sehemu za faragha, Aisha Abel, mama wa makamo ambaye alikuwa mwingi wa maneno alisema, “Hatuna vyoo, tunajisaidia kama mbwa wasio na kwao. Tunajisaidia kwenye vifusi... huko kwenye magofu. Usalama wetu kiafya si mzuri maana licha ya vyoo, hatuna hata maji na tunakaa gizani.”

Wahofia ndoa zao
Baadhi ya waathirika hao walisema wamelazimika kuzisafirisha familia zao kwenda vijijini na sasa wanahofia usalama wa ndoa zao.
“Nimesafirisha familia yangu yote kwenda kijijini kwetu mkoani Mtwara, nimebaki mimi mwanaume nikitafuta namna ya kuanza maisha upya,” alisema Chande Mohamed.

“Naishi hapa sina amani, maana lolote linaweza kutokea. Mke wangu yuko kijijini na watoto, mimi nimebaki hapa peke yangu. Hivi unategemea nini hapo kama si mwanzo wa kusalitiana,” aliongeza John Patrick.

Alisema kitendo cha kukaa mbali na familia yake kinamtesa kifikra kwa kuwa alizoea kukaa nao pamoja na kulala sehemu nzuri, lakini sasa analala nje tena kwenye hema kama mkimbizi.
“Acha kabisa haya maisha... kupitia hili janga kiukweli nimejifunza mengi. Sikia kwa mwingine tu yasikukute,” alisema.

“Mimi leo wakulala nje hivi! Acha tu dada yangu, sitaki kuongea chochote inaumiza sana” aliongeza Faustine John ambaye alisema ameiombea hifadhi familia yake kwa majirani.
“Mke wangu na watoto wanalala huko mimi nikitafuta namna ya kuanza upya maisha” alisema.

Salma aliyekuwa akisonga ugali alisema, “Sina makazi. Nyumba iliyobomolewa aliniachia urithi mume wangu ambaye ametangulia mbele za haki, hapo ndipo nilikuwa nikiishi na watoto wangu.”
Alisema yeye na watoto wake ambao ni wakubwa wanalala nje na wajukuu wake wanane amewaombea hifadhi kwa majirani.

Maisha ya kaya
Baada ya mazungumzo na waathirika wanaoishi katika mahema, waandishi wetu walifika katika kaya ya Halima Ramadhani ambaye ana watoto watatu na wajukuu wanane.

Wakati huo ilikuwa saa nne usiku na walimkuta, Halima ambaye alipoteza nyumba zake mbili akiwa anaota moto huku watoto wajukuu wake wakiwa wamelala kwenye mkeka karibu na moto aliokuwa akiota wakiwa wamefunikwa vitenge na khanga.

“Siku walipokuja kubomoa mimi sikuwepo nilitoka kwenda sokoni, na hata watoto wangu ambao ni wakubwa hawakuwepo, walibaki wajukuu zangu, sasa nikiwa ninakaribia nyumbani niliona watu wamekusanyika. Nikauliza nini hicho? Mmoja wa watu waliokuwa jirani akanijibu ‘Tanroads wanabomoa....’ Mwanangu nilihisi kuishiwa nguvu nikashindwa hata nifanye nini,” alisema.

Wakati wanabomoa alisema, hakubahatika kuokoa hata kitu kimoja.
Yote tisa, kumi ni hii familia ya watu 14 ya Bernard Mbonde ambayo imepoteza makazi na eneo lao lote lenye ukubwa wa eka nne yakiwamo makaburi ya familia kuwa katika hifadhi.

Waandishi wetu walipofika katika familia hiyo iliyopo Kibamba CCM saa sita usiku, walikaribishwa na ulinzi mkali wa mbwa ambao walibweka muda wote hali iliyowalazimu wanafamilia hao kuhofia kuwa huenda wamevamiwa na wezi.
“Jamani usalama upo? Mnatafuta nini usiku huu? Alihoji mmoja wa wanafamilia hao ambaye baadaye alijitambulisha kuwa anaitwa Ibrahim Aboud aliyekuwa macho usiku huo.

Baada ya waandishi kujitambulisha, aliwakaribisha na kuwapeleka eneo ambalo wanafamilia wenzake walikuwa wakiota moto. Huko walikuta nyumba ya familia hiyo ikiwa imetolewa mabati na milango na kubaki gofu. Vitu vyote vilikuwa nje, wanaume walilala nje ya kibaraza cha gofu hilo.

Walitandika godoro kubwa na kufunga neti. Wanawake na watoto walilala ndani ya kichumba kidogo ambacho kilikuwa hakina paa. Humo walilala watu 10 wakiwamo watoto na mama zao.

“Karibuni jamani, poleni na kazi hakika kazi yenu ni ngumu mnafanya kazi hadi usiku poleni sana,” alisema mmoja wa wanafamilia hao Moses Mbonde aliyekuwa akiota moto nje. Baada ya makaribisho, moto ulichochewa upya hali iliyosababisha kuwapo kwa mwanga mkubwa. Wakati wote huo bado mbwa waliokuwa wamefungwa kila upande wa nyumba hiyo waliendelea kubweka.

“Msiogope hawa mbwa tumewaweka kama walinzi, vitu vyetu vyote viko nje,” alisema Aboud.
“Tuna vitu vya thamani kusema ukweli, lazima tuvilinde, tuna mabati ya aluminiamu, mbao za mninga na madirisha. Tunachofanya tunapokezana kulala,” alisema Moses.

Moses alisema wamekuwa wakiishi maisha ya hofu na hata kutokupata usingizi.
“Tulizoea kulala ndani ya kiyoyozi leo tunalala nje tunaumwa na mbu inaumiza sana. Hata usingizi tunaoupata ni wa kuungaunga tu” alisema.

No comments:

Post a Comment

Popular