Vijana wa Zinedine Zidane timu ya Real Madrid imetwaa ubingwa wa Super Cup nchini Hispania kwa kuwatwanga mahasimu wao Barcelona jumla ya mabao 5-1.
Ushindi huo imepatikana baada ya Real kushinda mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza uliopigwa usiku wa Jumapili katika dimba la Camp Nou na kuhitimisha kwa ushindi wa 2-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa usiku wa kuamkia leo dimba la Santiago Bernabeu.
Waliopeleka msiba Barcelona katika mchezo huo wa marudiano ni yuleyule kijana aliyewaliza kwenye game ya kwanza Marco Asensio dakika ya 4 kabla ya Karim Benzema kumaliza kazi dakika ya 38 na kukabidhiwa rasmi kombe lao.
Katika mchezo huo wa marudiano, kwa mara ya kwanza Lionel Messi ameshindwa kufunga bao lolote katika mchezo wa Super Cup dhidi ya Real Madrid huku Barcelona wakishindwa kupata bao lolote katika michezo 25 dhidi ya Real Madrid.
Kocha Zinedine Zidane amefikisha ushindi wake wa 68 kati ya mechi 90 ambazo ameiongoza Real Madrid akiwa amepoteza mechi 7 pekee huku akitwaa taji lake la 7 kama kocha.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana katika mchezo wa Super Cup ilikuwa mwaka 2012 ambapo Real waliibuka mabingwa kwa bao la ugenini
Super Cup ni maalum kwa ajili ya ufunguzi wa msimu mpya wa mashindano nchini humo na huwakutanisha mabingwa wa La Liga ambao kwa msimu uliopita walikuwa ni Real Madrid na mabingwa wa kombe la mfalme ambao ni Barcelona.

No comments:
Post a Comment