Mbeya: Wananchi wauza mali zao na kujenga wodi ya wazazi - KULUNZI FIKRA

Tuesday 22 August 2017

Mbeya: Wananchi wauza mali zao na kujenga wodi ya wazazi

 
 Mbeya. Wakazi wa Kata ya Maendeleo Wilaya ya Mbeya, mkoani hapa wameamua kuuza mali zao ili kuchangia ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha afya Ikhoho ili kuwaepusha wanawake kujifungua kwenye mazingira magumu.

Wananchi hao wamefanya harambee ya kuchangia ujenzi huo na jumla ya Sh5 milioni zimepatikana huku gharama ya jengo hilo ikitarajia kufikia Sh73 milioni.

Wakizungumza kwenye harambee hiyo iliyofanyika katika kituo cha Afya Ikhoho, wananchi hao wamesema wajawazito wanapata shida wanapokwenda kituoni hapo kujifungua kwa kulazimika kujibanza kwenye chumba kidogo ambacho hakikidhi mahitaji muhimu.

Mkazi wa Maendeleo, Burton Maketa amesema wameamua kutoa fedha za mifukoni na kuuza mali zao ili kufanikisha ujenzi huo kutokana na adha wanayoipata wake zao wanapokwenda kujifungua kituoni hapo.

Katika harambee hiyo iliyojumuisha wakazi wa vijiji vinavyounda kata hiyo, jumla ya Sh5 milioni zimepatikana huku lengo likiwa ni kukusanya Sh73 milioni ambazo zitakamilisha ujenzi wa jengo hilo.

Mganga Mkuu wa Kituo hicho, Dk Jafar Leonard amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na wakazi hao lakini bado kituo kinakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na majengo ya kutosha.

Amesema wananchi wa kata hiyo wameonyesha uzalendo wa kujitafutia maendeleo badala ya kusubiri Serikali kwani mbali na ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi, awali pia walitumia rasilimali zao kujenga jengo la utawala ambalo kwa sasa lipo hatua za upauaji.

“Tunahitaji wodi ya wanawake, wanaume, watoto, jengo la upasuaji, chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na jengo la kuhifadhi dawa kwa ajili ya wagonjwa wanaotumia kituo hiki, na tunashukuru wananchi wa kata hii wameonyesha moyo wa kipekee kabisa kwa hiki wanachofanya kwa kujitoa kwao kuchangia maendeleo badala ya kusubiri Serikali na wadau wengine,’’ amesema Dk Leonard.

Dk. Leonard ambaye alikuwa katibu wa harambee hiyo alibainisha kuwa kipaumbele cha ujenzi wa jengo hilo kitasaidia wanawake wengi kujifungulia kituoni hapo na wakiwa katika mazingira salama.

Amesema kwa sasa inawawia vigumu pale inapotokea wajawazito watano kufika kituoni hapo kwa wakati mmoja wakihitaji kujifungua kwani chumba kilichopo hakikidhi haja wala hakina hadhi jambo linalowafanya kuwa kwenye mazingira magumu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Mwalingo Kiseba amesema hatua iliyochukuliwa na wananchi hao ni ya kizalendo na inaonyesha kwamba wametambua umuhimu wa kujiletea maendeleo wenyewe badala ya kusubiri Serikali huku akisisitiza uongozi wa halmashauri hiyo utawaunga mkono katika jitoihada zao.

Amesema ‘kata hii ina wananchi 800 wenye nguvu ya kufanya kazi na kila mwananchi akitoa Sh20,000 wanaweza kupata fedha nyingi hivyo akashauri wananchi kujinyima kufanya starehe ili kuleta maendeleo katika jamii.

Katika harambee hiyo, Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza alitoa Sh1 milioni kuunga mkono jitihada za wananchi hao, fedha ambazo ziliwakilishwa na mwenyekiti huyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya, Amelchiory Kulwizila amesema halmashauri inasimamia sera na kanuni za afya kwa ajili ya kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana kwa wananchi wote.

‘’Hili lipo kwenye sera yetu na ujenzi wa vituo vya afya ni mpango mkakati unaotekelezwa, hivyo mimi nitapigania gari ya kubebea wagonjwa itapatikana pamoja na kumalizia majengo ili huduma za kitabibu ambazo mnazifuata ,Igawilo Meta na Hospitali ya rufaa zianze kupatikana hapa,’’ amesema mkurugenzi huyo .

Amesema pamoja na halmshauri kuchangia fedha lakini itatoa mifuko 20 ya saruji kwa ajili ya kuanzia ujenzi huo na kwamba atakuwa bega kwa bega na wananchi hao ili kufanikisha jambo hilo.

No comments:

Post a Comment

Popular