Mafaili kesi ya Lema yapelekwa kwa DPP - KULUNZI FIKRA

Tuesday 22 August 2017

Mafaili kesi ya Lema yapelekwa kwa DPP

 
 Mahamaka ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arusha imeshindwa kusikiliza kesi namba 440/2016 na 441/2016 zinazomkabili mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema baada ya majalada kuitwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Kesi hizo za uchochezi jana zilifikishwa mahakamani kwa ajili ya Lema kusomewa maelezo ya awali, baada ya upelelezi kukamilika.

Hata hivyo, Mwanasheria wa Serikali Agnes Hiera aliiambia mahakama hiyo kuwa DPP ametaka majalada ya kesi hizo na hivyo isingewezekana kumsomea mbunge huyo kwa tiketi ya Chadema mashtaka yake.

Baada ya maelezo hayo, wakili wa utetezi, Sheck Mfinanga aliiomba mahakama iahirishe kesi hiyo kwa mara ya mwisho kwa kuwa imekuwa ikiahirisha mara kwa mara.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arusha, Devota Msofe aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 20.

Akizungumza nje ya mahakama jana, Lema alisema hajui hatma ya kesi hiyo kwa kuwa kupeleka majalada kwa DPP huenda wanataka kumuongezea mashitaka.

“Wamesema mafaili yameombwa na DPP tunasubiri labda wanataka kuongeza mashitaka iwe uhaini,” alisema.

Kutokana na kesi hizo, Lema alikaa mahabusu miezi minne kutokana na ubishani wa kisheria kuhusu dhamana yake.

Alikamatwa mjini Dodoma ambako alikuwa akihudhuria vikao vya Bunge Novemba mwaka jana na kusafirishwa hadi Arusha ambako alifikishwa mahakamani na licha ya hakimu kuweka wazi dhamana, upande wa mashtaka ulipinga hadi Mahakama Kuu ilipotengua.

Lema anadaiwa kutoa matamshi yenye chuki na kuibua nia ovu kwa jamii Oktoba 23 mwaka jana wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja vya Shule ya Sekondari Baraa.

Akinukuu maneno ya Lema wakati wa kumsomea mashtaka, wakili mwandamizi wa Serikali, Martenus Marandu alisema: “Kiburi cha Rais kisipojirekebishwa, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu, mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshachukua maisha yake.

“Rais ana kiburi, Rais kila mahali watu wanaonewa, wafanyakazi wa Serikali hawana amani, wafanyabiashara hawana amani, watu wananyanyaswa”.

Katika kesi nyingine, Lema anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi Oktoba 22 mwaka jana akiwa maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro wakati wa mkutano wa hadhara.

Anadaiwa kusema: “Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani iko siku Taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu.

“Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya Katiba, Rais huyo ataingiza Taifa katika majanga na umwagaji damu, watu watajaa vifua, wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.”

No comments:

Post a Comment

Popular