Kamati yaundwa kuchunguza tukio la moto Mbeya - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 16 August 2017

Kamati yaundwa kuchunguza tukio la moto Mbeya



Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika, ameunda kamati maalum ya kuchunguza chanzo cha moto ulioteketeza vibanda zaidi ya 2,000 katika soko la SIDO lililopo katikati ya jiji la Mbeya usiku wa kuamkia leo.

Hatua hiyo inafuatia chanzo pamoja na hasara iliyosababishwa na moto kutofahamika hadi sasa.

Naye mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ametoa pole kwa wote walioathirika na janga hilo lililoanza majira ya saa 3 usiku huku akiwashukuru wananchi na vyombo vya ulinzi na Usalama kwa ushirikiano na kazi kubwa ya kudhibiti moto huo usiendelee kuleta madhara makubwa zaidi.

“Serikali kupitia Mkuu wa wilaya ya Mbeya imeunda kamati ya kufanya tathmini ya kujua hasara na chanzo cha moto huo. Tunaomba wananchi waendelee kuwa watulivu na watoe ushirikiano kwa kamati hiyo ili tuweze kujua chanzo cha moto na hasara iliyopatikana,” Imeeleza sehemu ya taarifa ya Makalla.

Aidha Makalla amesema kuwa vyombo vya ulinzi vinaendelea kuchunguza kujua kama moto huo utakuwa umesababishwa na mtu au  watu.

Katika tukio hilo magari mawili ya jeshi la Zimamoto yalishindwa kuuzima kwa wakati kutokana na upepo mkali uliochagiza kuongeza kasi na kuzidi kuteketeza mali.

Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu soko hilo kuungua moto na mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2010 ambapo mali za wafanyabiashara ziliteketea na kujenga vibanda vipya.

No comments:

Post a Comment

Popular