Cuf washtukia mkakati wa kumng'oa Maalim Seif - KULUNZI FIKRA

Friday 25 August 2017

Cuf washtukia mkakati wa kumng'oa Maalim Seif

 
 Dar/Zanzibar. Jumuiya ya Wanawake wa CUF (JUKECUF), imedai ina taarifa za kuandaliwa kwa mkutano mkuu iliouita bandia wenye lengo la kupitisha azimio la kumvua uanachama katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Jumuiya hiyo inayomuunga mkono, Maalim Seif imesema mkutano huo upo mbioni kufanyika na unaandaliwa na upande unaomuunga mkono mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wakati JUKECUF ikitoa madai hayo, upande wa Profesa Lipumba kupitia kwa mkurugenzi wa uchaguzi na oganaizesheni, Nassor Seif umejibu mapigo na kusema hawana nia ya kumfukuza uanachama Maalim Seif na kwamba huo ni uvumi wa mitaani.

Mwenyekiti wa JUKECUF, Fatma Ferej aliibua taarifa hizo jana wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi ndogo za makao makuu ya chama hicho yaliyopo Vuga mjini Unguja.

Alisema hatua ya kumvua Maalim Seif uanachama ikikamilika, ajenda kuu ya mchakato huo ni kuiondoa CUF katika kusimamia madai yake ya ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 ambao matokeo yake yalifutwa.

“Tunazitahadharisha mamlaka za dola, ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba orodha kamili ya wajumbe halali wa Mkutano Mkuu wa CUF-Taifa ipo na inajulikana kama ilivyopatikana kupitia Uchaguzi Mkuu wa CUF wa mwaka 2014 na si vingevyo.

“Pia tuna taarifa baadhi ya waliowahi kuwa wabunge na nafasi za uongozi ndani ya CUF ndiyo wale wanaoongoza njama za kukusanya majina bandia ya wajumbe wa mkutano mkuu huu ili kukamilisha dhamira yao. Tunatoa wito kwa wanachama wetu kutowapa ushirikiano kabisa, ijapokuwa watatumia ghilba,” alisema Ferej.

Kuhusu wabunge wanane waliovuliwa uanachama na kukosa sifa za kuwa wabunge, Ferej alisema JUKECUF bado inaendelea kuwatambua wanachama hao na nafasi zao za ubunge na wana imani mahakama itatenda haki.

Wabunge hao ni Halima Ali Mohamed, Khadija Salum Ally, Salma Mohamed Mwasa, Miza Bakari Haji, Raisa Abdallah Mussa, Riziki Shahari Mngwali, Saumu Heri Sakala na Severina Mwijage.

“Njama hizi ovu zinazoendelea ni sawa na kumrejesha nyuma mwanamke wa Kitanzania katika harakati za siasa na zimekuwa zikifanyika siku hadi siku, ni lazima tupinge na kukemea iwapo tunatekeleza agizo la haki sawa kwa wote,’’ alisema Ferej.

Hata hivyo, Nassor aliwataka wana-CUF kupuuza taarifa hizo na kusema kinachofanyika sasa ndani ya chama hicho ni kuratibu shughuli za Mkutano Mkuu wa dharura utakaojadili ajenda mbalimbali ambazo hakuwa tayari kuziweka wazi akidai bado ni mapema.

“Ingawa sizitaji ajenda hizo lakini katibu mkuu wa chama kwa hatua yake ya kukataa kutoa ushirikiano wake kwa Profesa Lipumba ili chama kipige maendeleo na kuondokana na mizozo isiyokuwa na faida itajadiliwa,” alisema .

Alisema katika kikao hicho cha dharura wanatarajia kumpa mwaliko Maalim Seif ili ashiriki kama kiongozi na endapo atashindwa, wajumbe wa mkutano huo watakuwa na hiari juu ya hatua za kuchukua dhidi yake.

No comments:

Post a Comment

Popular