serikali yatangaza ajira 3,152 sekta ya afya. - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 25 July 2017

serikali yatangaza ajira 3,152 sekta ya afya.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo imetangaza ajira 3,152 kwa ajili ya wahitimu wa kada mbalimbali za afya nchini.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na wizara hiyo, ajira hizo ambazo zinatolewa kwa kibali cha wizara ya utumishi na utawala bora, ni kwa ajili ya watumishi kutoka kada 33 za afya.

Baadhi ya kada zilizotangazwa ni pamoja na madaktari, wataalam wa maabara, wauguzi/wauguzi wasaidizi, matabibu wasaidizi, wataalam wa meno, wataalam wa afya ya mazingira, wataalam wa mionzi, wataalam wa takwimu za afya, makatibu muktasi katika sekta ya afya, wataalam wa usafi, washauri wa afya, wafamasia n.k

Ajira hizo zinawahusu wahitimu wote wenye sifa stahiki za kitaaluma na hazitawahusu wahitimu wenye umri zaidi ya miaka 45, wahitimu ambao tayari ni waajiriwa wa serikali au wa mashirika wanaolipwa na serikali, pia hazitawahusu watu wote ambao wamewahi kufanya kazi serikalini na kuacha.

Ujio wa ajira hizi, ni tulizo la nafsi kwa wahitimu ambao wamekuwa wakisubiri ajira serikalini kwa takriban miaka miwili tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, ambayo mwaka jana ilisitisha ajira kwa ajili ya kupisha zoezi uhakiki wa watumishi hewa.

Pia ajira hizo ni kuanza kwa utekelezaji wa mipango ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 ambapo mara kadhaa imekuwa ikiahidi kutoa ajira zaidi ya 50,000.

Waombaji wote wametakiwa kutuma maombi yao kabla ya Agosti 11 mwaka.

No comments:

Post a Comment

Popular