MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ametoa pongezi alizosema ni za kipekee kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akisema anastahili kuigwa kwa kuwa ameimudu vyema wizara hiyo.
Alitoa pongezi hizo juzi wakati Lukuvi akizindua rasmi ramani mpya ya mipango miji ya Manispaa ya Iringa katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi wadau mbalimbali. “Kwa mnaonifahamu vizuri mimi sio mbunge wa kusifia-sifia, mimi ni mbunge mwenye msimamo, lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipotoa pongezi kwa Waziri Lukuvi kutokana na uchapakazi wake unaokonga nyoyo za wadau wa shughuli zinazofanywa na wizara yake,” alisema Mchungaji Msigwa.
Lukuvi alisema serikali imejipanga kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria, maofisa ardhi wanaofanya udanganyifu ili kujipatia fedha. Alisema moja ya udanganyifu unaofanywa na maofisa ardhi hao ni ule unaoonesha maeneo mazuri katika ramani zao kuwa ni maeneo yasiyofaa kwa ujenzi kwa kuwa si maeneo salama kumbe sio kweli. “Mchezo huu wa kifisadi umekuwa ukitumiwa kwa miaka mingi na umekuwa ukiwapa fedha nyingi kutoka kwa wale wanaohitaji maeno hao kwa sababu ya uzuri wake,” alieleza.
Aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri nchini kutozipokea ramani za maeneo mapya zinazoletwa na wataalamu wao bila kujiridhisha kwa kuyaona maeneo hayo. “Kuanzia sasa wote waliopo katika maeneo yasiyopimwa watapewa leseni ya makazi ya miaka mitano na watalipa kodi ya ardhi baada ya miaka mitano wahakikishe wamepimiwa ili kupewa hati,” alisema Lukuvi.
Akitoa taarifa ya uandaaji wa ramani mpya ya mipango miji kwa ajili ya mwaka 2015-2035, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Dk William Mafwere alisema dhumuni la mpango huo ni kutatua changamoto za masuala ya ardhi zilizokuwa zinaikabili manispaa hiyo. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema mkoa huo unaendelea kuwahamasisha wananchi kuzingatia sheria na taratibu za ujenzi ili kuwa na mji bora unaovutia.
No comments:
Post a Comment