Spika wa Bunge atoa masaa kwa Serikali kutoa ufafanuzi juu ya kupanda kwa bei ya Mafuta ya Kula. - KULUNZI FIKRA

Tuesday 8 May 2018

Spika wa Bunge atoa masaa kwa Serikali kutoa ufafanuzi juu ya kupanda kwa bei ya Mafuta ya Kula.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe  Job Ndugai ameishukia Serikali kuhusu madai ya kupanda kwa bei ya mafuta ya kula akimtaka Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe Charles Mwijage kufikia leo Jumanne Mei 8, 2018 saa 11 jioni kuwasilisha bungeni taarifa ya kinachoendelea kuhusu jambo hilo ili kuondoa sintofahamu kwa wananchi.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo asubuhi bungeni mjini Dodoma wakati akijibu mwongozo wa mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Mhe  Hussein Bashe aliyehoji kuhusu bei ya mafuta, akidai imepanda na kujibiwa na Mwijage kuwa jambo hilo linashughulikiwa kwa maelezo kuwa kwa sasa umeibuka mvutano.

Tishio la kuadimika kwa mafuta ya kula linatokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzizuia meli mbili zenye tani 62,000 za mafuta ya kula katika Bandari ya Dar es Salaam tangu mwezi uliopita kushusha mzigo mpaka wamiliki wake watakapolipa kodi husika.

Utata wa kulipa kodi inayodaiwa na TRA, unatokana na madai ya mamlaka hiyo inayosema mafuta yaliyoingizwa ni safi ilhali wamiliki wakieleza ni ghafi.

Leo katika majibu yake, Mhe Mwijage baada ya kutoa maelezo marefu amesema alitoa ushauri kwa TRA kwamba wenye mafuta, “nusu ya mzigo ushushwe, tatizo linalokuja tunahukumiwa na historia, nashauri hii kazi unipe mimi, nitakuja saa 11 kukueleza kipi kimetokea.”

Baada ya kauli hiyo ya Mhe Mwijage, Spika Ndugai alisimama na kusema: “Nalikubali hili la saa 11 na bahati nzuri nitakuwa hapa. Tunapokuwa bungeni lazima tuseme ukweli yaani iko hivyo.Tukiligeuza Bunge hili kuwa mahali pa kubangazia hivi, mimi niombe saa 11 tupate majibu ya uhakika.”

“Mnatufikisha mahali pagumu sana, kwa mambo madogo mno, hivi tuliosoma kemia hivi kupima mafuta kujua ni ghafi au masafi inachukua muda? Kitu cha dakika kumi na tano watu wanazunguka zunguka. Hamuwamini TBS (Shirika la Viwango Tanzania) au pelekeni Nairobi, Afrika Kusini, Kenya mnapima na kupiga kodi.”amesema Spika Ndugai.

Huku akishangiliwa Spika  Ndugai amesema, “…tunaumiza wananchi na hata yakikaa huko yakiingia anayeumia ni mwananchi, sisi tunalumbana tu.”

Awali, baada ya majibu ya Mhe  Mwijage, Spika  Ndugai alimtaka mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira,Mhe  Suleiman Saddiq kulielezea suala hilo na kusema walipokutaka katika semina Jumamosi iliyopita, lilijitokeza ukiwamo mkanganyiko kati ya TBS, TRA na Mkemia Mkuu wa Serikali.

Baada ya Spika  Ndugai kueleza msimamo wake kuhusu jambo hilo,  Mhe Mwijage alinyanyuka alipokuwa ameketi kwenda kuteta na waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe Jenista Mhagama kisha kwa pamoja kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.

             
                     Bei ya Sukari yatikisa Bungeni.

Spika wa Bunge Job Ndugai amelazimika kuingilia kati mvutano ulioibuka bungeni kuhusu tofauti ya bei ya sukari kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa maelezo kuwa majibu yaliyotolewa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage juu ya jambo hilo hayajajitosheleza.

Kufuatia sakata hilo, Spika Ndugai amesema swali hilo litaulizwa tena wiki ijayo ili Serikali itoe majibu ya kina, “hili ni swali la msingi sana na linapaswa kutolewa majibu mazuri na Serikali.”

Mvutano huo ulitokana na swali la mbunge wa Mpandae (CCM), Mhe Salim Hassan Turky aliyehoji tofauti ya bei hizo na kujibiwa na Mwijage, majibu ambayo mbunge huyo hakuridhika nayo.

Katika maelezo yake Mwijage amesema Tanzania Bara haina uhaba wa sukari na kuwatoa hofu watu mbalimbali.

Kuhusu tofauti ya bei kwa pande mbili za muungano, waziri huyo  amesema zaidi ya asilimia 53 ya sukari itumikayo Zanzibar huagizwa kutoka nje kwenye vyanzo ambavyo gharama zake ni nafuu ikilinganishwa na asilimia 29 ya sukari inayoagizwa nje  kwa upande wa bara.

Kufuatia majibu hayo Spika  Ndugai amesema swali hilo halikujibiwa vyema. Katika swali la msingi  Mhe Jaku Hashim Ayoub (BLW) alihoji juu ya tofauti ya bei ya bidhaa hiyo katika pande hizo mbili za muungano na kubainisha kuwa gunia la kilo 50 visiwani Zanzibar linauzwa kwa Sh65,000 huku gunia hilo kwa upande wa Tanzania Bara likiuzwa kwa Sh120,000.

Katika majibu yake ya swali la msingi, Mhe Mwijage amesema wametoa maagizo kwa viwanda vinne vya kuzalisha sukari nchini kuongeza ulimaji wa miwa katika mashamba yake.

“Bei ya sukari ina maana kubwa kwa maisha ya Watanzania, haiingii akilini bei ya Tanzania Bara kuwa tofauti na ile ya Zanzibar,” amehoji Spika  Ndugai.

No comments:

Post a Comment

Popular