Mwanafunzi achomwa moto na Walimu Wake. - KULUNZI FIKRA

Tuesday 8 May 2018

Mwanafunzi achomwa moto na Walimu Wake.

Mwanafunzi wa kidato cha pili Sekondari ya Kayanga wilayani hapa mkoani Kagera, anadaiwa kufanyiwa ukatili na walimu wake kwa kupigwa na kuchomwa moto viganja vya mikono na miguuni kwa madai ya kutoroka bwenini.

Tukio hilo linalodaiwa kufanywa na walimu wawili lilitokea Mei 4 shuleni hapo kwa kumchapa viboko na kummwagia moto kwa kutumia koleo.

Mkuu wa shule hiyo, Johnbosco Paul alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba asingependa kulizungumzia kwa kuwa tayari limefikishwa polisi.

Ofisa ustawi wa jamii Wilaya ya Karagwe, Owokusiima Kaihura alisema alipata taarifa za mwanafunzi huyo kuwa amelazwa zahanati binafsi ya Family kutokana na kuunguzwa moto na walimu wake.

“Nilipofika kwenye zahanati hiyo nilimpeleka katika Kituo cha Afya Kayanga kisha nikatoa taarifa polisi kuhusu tukio hilo. Nitaendelea kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo,” alisema Kaihura.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Mchungaji Upendo Simba alisema: “Nimesikitishwa na kitendo cha mwanangu kuunguzwa moto, naiachia polisi ifanye kazi yake, mume wangu amesafiri akirudi tutaona cha kufanya iwapo tumhamishe shule au la,” alisema.

Alipotafutwa mkuu wa Kituo cha Polisi Kayanga, Mika Makanja ili kuzungumzia suala hilo licha ya kukiri kuwapo kwa tukio hilo, alisema hawezi kulitolea ufafanuzi kwa sababu yupo nje ya kituo cha kazi.

Waraka wa Wizara ya Elimu kuhusu utoaji adhabu kwa wanafunzi, unataka warekebishwe tabia ili wawe viongozi wazuri.

No comments:

Post a Comment

Popular