Miili ya askari waliokufa nchini Congo kurejeshwa nchini. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 10 December 2017

Miili ya askari waliokufa nchini Congo kurejeshwa nchini.

Serikali inashirikiana na umoja wa mataifa (UN) kuhakikisha miili ya askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliouwa na waasi katika jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) inarejeshwa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jumapili Desemba 10, 2017 jijini Dar es salaam mnadhimu mkuu wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) Luteni Jenerali James Mwakibolwa amesema miili ya askari hao itarejeshwa nchini kati ya Jumanne Desemba 12 na Jumatano Desemba 13, 2017.

Mwakibolwa amesema askari hao walivamiwa kambini na waasi wa ADF na mapingano yalidumu kwa saa 13.

Mwakibolwa amesema askari 14 wa JWTZ waliuawa, 44 wamejeruhiwa na wengine wawili hawajulikani walipo.

Mwakibolwa amesema tukio hilo lilitokea Desemba 7, 2017 katika kambi mdogo iliyopo katika daraja la mto Simulike, Kaskazini mashariki mwa Wilaya ya Ben, Jimbo la Kivu.

Mwakibolwa pia amesema shambulio hilo ni kubwa zaidi kutokea tangu JWTZ  ianze kushiriki ulinzi wa amani nchini Congo mwaka 2011.

"Taarifa za kusafirisha miili ya marehemu kuirejesha nchini inafanyika chini ya uratibu wa serikali ya umoja wa mataifa. JWTZ na serikali tunaendelea kuchukua hatua sitahiki kufuatilia tukio hilo ikiwemo kufanya uchunguzi katika eneo husika", amesema Mwakibolwa.

Amesema tukio hilo halitawavunja moyo JWTZ wala kutetereka kupeperusha bendera ya Tanzania ndani na nje ya nchi bali linawaongezea ari, nguvu, ushupavu na uhodari zaidi katika kutekeleza majukumu ya yao.

"Ni bahati mbaya mashujaa wetu wameuawa wakiwa wanatekeleza jukumu la ulinzi wa amani nchini Congo. Kwa umoja Watanzania tuwaombee dua roho zao zipumzike kwa amani na majeruhi wapone haraka iwezekenavyo ili warejee kuelekeza majukumu yao", amesema Mwakibolwa.

No comments:

Post a Comment

Popular