Maalim Seif aungana na Rais Dkt John Magufuli. - KULUNZI FIKRA

Saturday, 9 December 2017

Maalim Seif aungana na Rais Dkt John Magufuli.

 
 Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, ameungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, katika kuomboleza vifo vya askari 14 waliouawa nchini Kongo na wengine kujeruhiwa, huku akiwapa pole wafiwa wote.

Kufuatia msiba huo Maalim Seif ametuma salamu za rambirambi kwa Rais Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, Maafisa na Askari wote wa JWTZ, familia na ndugu wa marehemu na Watanzania wote kwa ujumla, kwa kuwapoteza mashujaa waliokuwa wakitekeleza wajibu wao kwa niaba ya Taifa.

"Natuma salamu zangu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa waathirika wote na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na kwa wale waliojeruhiwa nawatakia uponaji wa haraka ili warejee katika majukumu yao ya kawaida, na tunawaombea marehemu wote Mwenyenzi Mungu awapumzishe mahala pema peponi", amesema Maalim Seif.

Pamoja na hayo Maalim Seif amesema anaungana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kulaani shambulio hilo, na kuitaka nchi ya Congo kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo, na kuwachukulia hatua wale waliohusika.

“Tunaungana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kulaani shambulio hilo ambalo ni sawa na uhalifu wa kivita, na kuitaka DRC Congo kufanya uchunguzi kuhusu shambulio hilo na wahusika wote kuchukuliwa hatua stahiki na kuwajibishwa", amesema Maalim Seif.

Hapo Jana imetolewa taarifa kuwa askari 14 wa Tanzania wa kulinda amani nchini Kongo wameuawa, huku 44 wakiwa majeruhi, 8 miongoni mwao wakiwa mahututi, na wawili hawajulikani walipo.

No comments:

Post a Comment

Popular