Kiongozi wa CCM awanyooshea kidole viongozi wa serikali kwa kuingilia uchunguzi wa chama. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 7 December 2017

Kiongozi wa CCM awanyooshea kidole viongozi wa serikali kwa kuingilia uchunguzi wa chama.

Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Arusha ,ndugu Loata Sanare amewanyooshea vidole baadhi ya viongozi wa mkoa wa Arusha kwamba walitaka kuingilia uchunguzi ndani ya chama na kushiriki kupanga safu zao.

Amesema katika uongozi wake wa kipindi cha miaka mitano, hatapenda kuona mambo hayo yakiendelea kujitokeza katika chaguzi zijazo, pia aliwashauri viongozi hao wa serikali kumsaidia Rais Magufuli katika utekelezaji wa Ilani ya chama cha mapinduzi (CCM).

Sanare bila kutaja majina ya viongozi hao amesema serikali inapaswa kuachana kuingilia uchunguzi wa CCM ili wanachama wachague watu wanaowataka.

"Tumeingiliwa na watu wanataka kutuchagulia viongozi wa CCM wanaowataka wao kitu ambacho sio kizuri, viongozi wetu wa serikali ndani ya mkoa na wilaya tunapofanya Uchaguzi ndani ya chama watuachie tuchague watu tunaowataka na sio wanaowataka wao", amesema Sanare.

Msimamizi wa uchaguzi huo, ndugu  Stephen Wasira alitangaza matokeo ya Uchaguzi jana jumatano Desemba 6,2017 usiku alimtangaza Sanare Mshindi wa nafasi ya Uenyekiti wa mkoa wa Arusha kwa kupata kura 454 dhidi ya upinzani wake wa karibu ndugu Lekule Leiser aliyepata kura 352 na Juma Lasini aliyepata kura 12.

Wasira pia aliwataka wanachama kuwa kitu kimoja ili kuendelea kujenga chama na kufanya kazi bila makundi ili kuweza kuepusha migogoro ya Mara kwa Mara inayojitokeza mkoani Arusha.

Laiser aliwashukuru wajumbe wote waliompigia kura akisema ni lazima wajifunze kukubaliana na matokeo ili kuepusha makundi ndani ya chama ili kuendelea kuimarisha chama.

Pia wajumbe walimchagua Daniel Awakii kutoka wilayani Karatu kuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM (NEC) na Shaban Mdoe ambaye ni mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru kuwa katibu wa mwenezi wa mkoa wa Arusha.

No comments:

Post a Comment

Popular