Zitto kabwe ataja orodha ya watu waliopotea Mkuranga. - KULUNZI FIKRA

Friday, 4 May 2018

Zitto kabwe ataja orodha ya watu waliopotea Mkuranga.

 
Mbunge wa Jimbo la  Kigoma Mjini, Mhe Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) ameitaka Serikali kutoa majibu ya kupotea kwa watu 348 kwa zaidi ya miezi 11 katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji zote za mkoa wa Pwani huku akieleza kuwa 68 kati yao wanahofiwa kufa.

Mhe Zitto ametoa kauli hiyo leo Ijumaa May 4, 2018, wakati akichangia hoja ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kusema usalama wa raia umekuwa mashakani na hakuna uhuru wa watu kujieleza.

“Mhe mwenyekiti, tunataka Serikali ituambie kuna nini katika wilaya za Kusini, hapa nina orodha ya watu waliopotea na nitaomba nikukabidhi, hali ni mbaya mbaya kweli,” amesema Mhe  Zitto.

Mbunge huyo amesema ibara ya 15 kifungu cha pili kinampa nafasi kila mtu ndani ya Jamhuri ya Muungano kuwa na haki ya kuishi lakini anashangazwa na kusahaulika kwa hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere ya mwaka 1987.

Mhe Zitto alinukuu hotuba hiyo akisema; “Panapokuwa hapana haki wala imani na matumaini ya kupata haki, hapawezi kuwa na utulivu na badala yake panazuka fujo.”

Mhe Zitto pia amehoji ni kwanini Serikali imetenga asilimia 65 ya bajeti hiyo lakini polisi wameshindwa kutoa majibu ya moja kwa moja kuhusu uchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida, Mashariki Tundu Lissu

“Lakini ni miaka miwili Ben Saanane haonekani na hakuna majibu, Azory Gwanda haonekani na mke wake amezaa lakini mtoto hamjui baba, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo Diwani Kanguye haonekani na mama yake amekufa hata hajui mwanawe yuko wapi,” amesema Mhe Zitto.

No comments:

Post a Comment

Popular