Wabunge wa CCM wahoji sababu za kutokupanda kwa Mishahara ya Wafanyakazi. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 2 May 2018

Wabunge wa CCM wahoji sababu za kutokupanda kwa Mishahara ya Wafanyakazi.

 
Wabunge wa CCM, Mhe Sixtus Mapunda (Mbinga Mjini) na Mhe  Mussa Sima (Singida Mjini) wameitaka Serikali kutoa majibu ya lini wafanyakazi wataongezewa mishahara ili kuwakwamua wananchi kiuchumi.

Wabunge hao wamehoji hayo leo Mei 2, 2018 bungeni Jijini  Dodoma wakati wakiomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, Mhe Andrew Chenge wakitumia kanuni ya 67 (8) baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.

Mhe Mapunda amesema; “…kwa kuwa kuondoa umaskini wa kipato, kuna uhusiano wa moja kwa moja na ongezeko la mishahara ya watumishi wa Serikali wa pande zote. Na kwa kuwa jana siku ya Mei Mosi Rais (John Magufuli) aliji ‘commit’ kuwa ongezeko la mishahara pamoja na mambo mengine litazingatia hali halisi ya uchumi, uwezo wa taifa na uwezo halisi wa Serikali.”

“Na kwa kuwa ameji ‘commit’, Serikali inatoa kauli gani lini mishahara hiyo itapanda kwa sababu suala hili jana limeacha sintofahamu kwa wananchi,” ameongeza Mhe Mapunda.

Naye Mhe Sima licha ya kumpongeza Rais Magufuli kwa hotuba aliyoitoa jana mjini Iringa amesema; “Lakini kama bunge, tungetaka kujua ni lini sasa watumishi hawa watapandishiwa mishahara.”

Akitoa majibu ya miongozo hiyo ya wabunge, Mhe Chenge amesema Jana hata yeye alimsikiliza vizuri Rais Magufuli akielezea suala hilo.

Mhe Chenge amesema:  “Rais alisema hali ikiwa nzuri ataongeza mshahara na ataongeza kikweli kweli.

"Kwa kuwa ni swali ambalo linahusu na maslahi ya wafanyakazi wa Watanzania, ndiyo maana limelengwa na Mapunda na Sima, nadhani serikali mnaweza kupata nafasi nzuri ya kujielezea na kuwapa matumaini wananchi", amesema Mhe Chege.

“Ni lini, hayo ni maswali sasa tunaiachia serikali hadi hali ya uchumi itakaporuhusu, tufanye haya makubwa yatakayowezesha kukuza uchumi wetu kwa haraka siri ya maendeleo ni hiyo tu, tufanye kazi kwa bidii tukuze uchumi, lakini serikali nadhani kwa wakati muafaka wanaweza kulitolea maelezo,” amesema Mhe  Chenge.

No comments:

Post a Comment

Popular