Nape Nnauye awaendesha Mawaziri Sita. - KULUNZI FIKRA

Friday, 18 May 2018

Nape Nnauye awaendesha Mawaziri Sita.

Mbunge wa Jimbo la  Mtama (CCM), Mhe Nape Nnauye juzi aliwaendesha mawaziri sita aliposhikilia shilingi ya Waziri wa Kilimo, Dkt  Charles Tizeba baada ya kutoridhishwa na majibu ya Serikali kuhusu fedha za ushuru wa mauzo ya nje ya korosho.

Mchana, akichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2018/19 kabla ya jioni kushikilia shilingi ya waziri huyo, Mhe Nape alitaka kuondolewa kwa bajeti hiyo ili kuipa fursa Serikali kupitia vipaumbele vyake kabla ya kuiwasilisha.

“Nikiikubali bajeti hii, wakulima wa korosho, mbaazi, ufuta, pamba na wengineo, watanishangaa. Pamoja na hayo, naangalia ilani ya CCM ambayo baadhi yetu hawataki tuinukuu, naona inapingana na bajeti hii", alisema Mhe Nape.

“Kwa hiyo, tuishauri Serikali irudi mezani, iende ikaipitie upya na kuweka vipaumbele vya wananchi,” alisema Mhe  Nape.

Mhe Nape alihoji ni mahali gani zinakokwenda fedha pindi Serikali inapobana matumizi na pia fedha hizo zinakwenda wapi kila Serikali inapoongeza makusanyo ya mapato. Mbunge huyo alionyesha kutoridhishwa na vipaumbele vya Serikali kwa kile alichosema imekuwa ikitumia fedha nyingi katika miradi mikubwa inayoweza kujiendesha yenyewe na kushindwa kuwekeza fedha za kutosha katika miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Bunge lilipokaa kama kamati kupitia bajeti hiyo, Mhe Nape aliinuka akiomba kupatiwa maelezo ya Serikali kwenye suala la pembejeo na hasa majibu kuhusu ushuru wa mauzo nje (export levy).

“Kama majibu yataendelea kutoridhisha nitakamata shilingi kwa sababu hadi vikwazo hivi vitakapokwisha wakulima watakuwa wamemaliza msimu wa korosho,” alisema Mhe Nape.

Waziri Dkt Tizeba akijibu alisema Serikali imechukua hatua kadhaa kuhusu kupatikana kwa salfa kwa ajili ya mikorosho.

Dkt Tizeba alisema wizara itasimamia mtu yeyote asiuze salfa kwa zaidi ya bei elekezi iliyopangwa ya Sh32,000 kwa kilo 50.

“Hadi ninapozungumza, tani 7,680 za salfa zimeshaingia na kati ya hiyo tani 1,320 imeshagawanywa kwa wakulima. Na wiki hii tutaanza kugawanya katika maeneo ambayo korosho imetoa maua,” alisema Dkt Tizeba.

Mhe Nape alisimama akisema Serikali haielewi ukubwa wa tatizo hilo na kuomba kutoa hoja kwa wenzake kumuunga mkono kuchangia katika jambo hilo.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wa CCM na wa upinzani, akiwamo wa Mtwara Vijijini (CCM), Mhe Hawa Ghasia aliyesema makubaliano ya wadau na Serikali ni kuwa asilimia 65 ya mauzo ya korosho nje iende katika mfuko wa kuendeleza zao hilo. Alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 fedha hizo hazikupelekwa na kwa baadhi ya maeneo wameanza kupuliza salfa.

Mbunge wa  Jimbo la Lulindi (CCM), Mhe Jerome Bwanausi alisema Serikali inaonekana haijawa makini katika kuendeleza zao hilo na kama haitatoa fedha itaathiri uzalishaji wa korosho.

Wabunge wengine waliochangia ni  Mhe Cecil Mwambe (Ndanda -Chadema); Mhe Katani Katani (Tandahimba - CUF); na  Mhe Omary Mgumba (Morogoro Kusini Mashariki -CCM).

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Abdallah Ulega ambaye ni mbunge wa Mkuranga alitetea shilingi ya Waziri Tizeba akisema ni mkulima wa korosho anafahamu umuhimu wa pembejeo hizo.

“Nakuomba ndugu yangu Nape muda hauko pamoja nasi ni kweli korosho ina taratibu yake kwa kuhakikisha palizi. Kuna mfanyabiashara Abas Export wa pale jijini Dar es Salaam anauza mfuko (wa sulfa) wa kilo 50 kwa Sh32,000. Tutakapozuia shilingi mchakato utachelewa zaidi,” alisema Mhe Ulega.

Naibu waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe  Kangi Lugola alisema Serikali si ya kutilia shaka na kumtaka Nape kuamini mambo yote yatakwenda kufanyika.

Naibu waziri wa Fedha na Mipango, Dkt  Ashatu Kijaji alisema Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha wakulima wa korosho wanapata pembejeo kwa muda.

Mhe Kijaji alitoa mfano wa Sh7 bilioni zilizotolewa kwa utafiti, kati ya hizo Sh2.5 bilioni zinakwenda kulipa posho (honoraria) na Sh1.3 bilioni zilitumika kulipa posho na Sh1.35 bilioni kwa ajili ya uratibu.

Naibu waziri alisema kutokana na shaka, Serikali imelazimika kufanya tathmini na uhakiki kabla ya kuendelea kutoa fedha ili kuhakikisha wanaonufaika ni wakulima wa korosho.

Naibu waziri wa Wizara ya Kilimo,Mhe  Mary Mwanjelwa alimuomba Nape kuachia shilingi ya mshahara wa waziri akisema licha ya kutotolewa fedha kupisha uhakiki, wizara imejiongeza kwa kuhakikisha salfa inapatikana.

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge), Mhe  Jenista Mhagama alishauri kutumika kanuni ya 105 inayotoa nafasi ndani ya siku sita kabla ya bajeti kuu, kamati ya bajeti kukutana na Serikali na kufanya majumuisho ya bajeti za wizara zote.

“Acha tupitishe bajeti, tunazo siku sita za kuendelea kuzungumza mambo ambayo yamejadiliwa katika bajeti za wizara zote azitumie siku hizo. Namuomba mheshimiwa Nape amrudishie shilingi mheshimiwa waziri,” alisema Mhe Mhagama.

Mwenyekiti wa Bunge, Mhe Mussa Zungu alisema siku sita ni mbali, aliagiza Kamati ya Bajeti ikae jana na Nape aipeleke hoja yake hiyo kwenye kikao hicho kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.

“Siku sita ni mbali, naomba mheshimiwa Nape umrudishie waziri shilingi yake. Naagiza Kamati ya Bajeti mkae kesho (jana) na Nape atakuwa mgeni rasmi mumsikilize,” alisema Mhe Zungu.

Baada ya kauli hiyo, Mhe Nape alikubali uamuzi huo na kurejesha shilingi kwa sharti kuwa, wasipoelewana ndani ya kamati atarudi bungeni ili washughulikiane.

“Ninakushukuru kwa busara zako mwenyekiti, vinginevyo ningeendelea kung’ang’ania shilingi yake maana kuacha hivihivi ni kuwasaliti wakulima wa korosho. Huko hatutakwenda kufanya blabla, vinginevyo tutarudi hapa kushughulikiana korosho ndiyo siasa kule kwetu,” alisema Mhe Nape.

Alipotafutwa jana Mhe  Nape alikiri kwenda katika kikao cha kamati ya Bunge ya bajeti lakini alikataa kusema walichokubaliana, akitaka atafutwe Ghasia ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo.

Hata hivyo, Mhe Ghasia alipopigiwa simu yake ya mkononi, iliita bila kupokewa na baadaye alituma ujumbe mfupi wa maneno (sms) akisema ana shughuli nyingi kwa wakati huo na kuomba kutumiwa ujumbe.

Alipotumiwa ujumbe kutaka kujua kama walifikia muafaka katika hoja ya Nape hakujibu.

No comments:

Post a Comment

Popular