Musukuma afunguka mazito kuhusu waziri wa kilimo. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 16 May 2018

Musukuma afunguka mazito kuhusu waziri wa kilimo.

 
Unaweza kusema mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka 2018/19 ni moto kutokana na michango ya wabunge mbalimbali.

Jana Mei 15, 2018 katika mjadala huo mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Mhe Joseph Musukuma amemtaka Waziri wa Kilimo, Dkt Charles Tizeba kama ameshindwa kuisimamia vyema wizara hiyo aachie ngazi.

“Wewe ni jirani yangu ukienda katika Jimbo la Geita hakuna ghala hata moja la kununulia pamba, nikuulize mnapoweka masharti ya ushirika wainunue wapi?”amehoji Mhe Musukuma.

Mhe Musukuma amesema wamefanya kazi kubwa kuwahamasisha wakulima wa pamba lakini kitendo cha kuweka ushirika aliodai hauna tofauti na uliopita unawanyonya wakulima.

“Labda Rais (John Magufuli) na waziri mkuu (Kassim Majaliwa) hawakuupokea ushauri, haujawa mzuri kwani ulivyokuwa huko nyuma siyo. Ushirika uliopo sasa hivi ni wale wale, wamejibadili. Serikali na michango ya wabunge mmeiona, kesho asubuhi (leo) uje na kauli ya kuondoa ushirika kwa sasa ili tuuweke mwaka ujao,” amesema Mhe  Musukuma.

“Kuna watu wanalalamikia mahindi, mahindi tulishakosea, pamba iko sokoni.”amesema Mhe Musukuma.

Huku akishangiliwa, Mhe Msukuma amesema suala la mawakala kulipwa fedha zao lifikie mwisho, “Waziri wewe ni shahidi kuna tatizo gani kuwalipa mawakala, uhakiki gani usioisha, tueleze pesa haipo ili kama Bunge linaweza kukuombea, kuna watu wamekufa. Nyumba zao zinauzwa.”

Mhe Musukuma alimaliza kuchangia kwa kusema, “Kama hii kazi ni ngumu, njoo ukae huku nyuma uwasaidie mawaziri wakijibu."

No comments:

Post a Comment

Popular