Mbunge wa CCM afunguka kuhusu watoto wa vigogo na viongozi wanaotafuna fedha za Miradi ya Maji. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 9 May 2018

Mbunge wa CCM afunguka kuhusu watoto wa vigogo na viongozi wanaotafuna fedha za Miradi ya Maji.

 
Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini (CCM), Mhe  Ali Keissy amesema baadhi ya viongozi na watoto wa vigogo nchini wanatafuna fedha za miradi ya maji na kwamba, wamekuwa wakimfuata na kumuomba asiwataje hadharani.

Akizungumza katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji mwaka 2018/19 jana Jumanne Mei 8, 2018, Keissy ambaye Spika Job Ndugai alimpa dakika 15 za kuchangia badala ya 10, amesema kuna miradi mingi ambayo mikataba imeingiwa kiujanja ujanja na kindugu na kusababisha fedha kutafunwa bila utekelezaji wowote.

Huku Spika Ndugai akimtaka azungumze zaidi kwa maelezo kuwa anaonekana kuwa na uchungu mkubwa, Keissy amedai anawajua watafunaji wote wa fedha hizo na kwamba wamewahi kumuita wakimuomba anyamaze, lakini ameendelea kupaza sauti yake, kufanikiwa kuokoa Sh3 bilioni zilizotaka kutafunwa.

“Miradi mingi ya Mkoa wa Rukwa imeingiwa na kandarasi hovyo bila kufuata utaratibu, kuna mtu alichimba kisima  kwa gharama ya Sh300 milioni lakini ghafla akapewa Sh900 milioni. Wizi mtupu ndiyo maana nilimwambia mkurugenzi wa Takukuru akapige kambi Rukwa,” amesema  Mhe Keissy na kuongeza:

“Viongozi wakubwa ndiyo wenye miradi hiyo na wamekuwa wakinitafuta ili kuninyamazisha. Niliwaambia sipo tayari kunyamaza hata kidogo wakati wananchi wanaendelea kuumizwa, mmoja ni mtoto wa kigogo kama alivyomtaja Mhe Ester Bulaya (Bunda Mjini).”amesema Mhe Kessy.

No comments:

Post a Comment

Popular