Waziri afikiria Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2020. - KULUNZI FIKRA

Saturday, 21 April 2018

Waziri afikiria Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2020.

Ikiwa imesalia miaka miwili kabla ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kufanyika, baadhi ya wanasiasa visiwani Zanzibar wameanza kuweka wazi dhamira zao za kuwania nafasi ya Urais.

Mmoja wa wanasiasa hao ni Mwenyekiti wa Chama cha AFP, Mhe  Said Soud Said ambaye hivi sasa ni Waziri asiyekuwa na wizara maalumu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mhe Said Soud alisema kwamba ataendelea kugombea nafasi ya urais viswani Zanzibar na haitakua mara ya mwisho.

Pia Mhe Said Soud alisema lengo kuu la kugombea nafasi hiyo ni kutaka kubadilisha hali za wananchi ambao wanahitaji mabadiliko ya kiutawala.

Aidha Mhe Said Soud alisema umefika wakati wa Chama cha AFP kutawala Zanzibar.

“Ingawa kipindi kilichosalia hadi kufikia uchaguzi mkuu ni kirefu, lakini naamini hata ufanyike kesho nipo tayari kushiriki kwani uwezo ninao,” alisema Mhe Said Soud.

Mhe Said Soud aliwaasa viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani kuacha tabia ya ubinafsi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa wananchi ili kuona upinzani unafanya vizuri katika chaguzi.

Hata hivyo Mhe Said Soud alisema ifike wakati wananchi watumie akili zao kuamua na si kuamuliwa na baadhi ya wanasiasa kama ilivyo sasa kwa baadhi ya vyama vya upinzani.

“Ifike wakati wananchi muwapime wanasiasa wanapokuja kwenye kuomba ridhaa ikiwamo kujua malengo yao kwa sababu wengine wana malengo ya kuwatia kwenye ugomvi wa kisiasa usio kuwa na faida kwao,’’ alisema Mhe Said Soud.

Vile vile Mhe Said Soud aliwataka wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kujenga utaratibu mpya wa kuhoji viongozi wao sambamba na kutazama zaidi sera za maendeleo kwa maslahi ya nchi yao.

No comments:

Post a Comment

Popular