Wasanii wakutana kujadili taratibu za Mazishi ya kifo cha Agnes Masogange. - KULUNZI FIKRA

Saturday, 21 April 2018

Wasanii wakutana kujadili taratibu za Mazishi ya kifo cha Agnes Masogange.

 
Wasanii wa muziki wa kizazi kipya na filamu, jana walikusanyika viwanja vya Leaders Club kujadili namna watakavyosimamia taratibu za msiba wa msanii aliyekuwa akipamba video za muziki (video queen), Agnes Gerald maarufu kama Masogange.

Masogange alifariki dunia jana katika Hospitali ya Mama Ngoma iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Mmoja wa wasanii wa vichekesho nchini, Steve Nyerere alipoulizwa kuhusu msiba huo alisema wasanii watakutana Leaders Club kwa ajili ya taratibu za msiba huo.

“Kifo hiki kimetushtua sana, wasanii wote bado hatujajua cha kufanya, hivyo tunakutana kwa ajili ya kikao cha dharura kupanga kuhusu msiba huu,” alisema.

Awali, taarifa za kifo cha Masogange zilithibitishwa na mwanasheria wake, Reuben Simwanza aliyesema aliambiwa na dada wa marehemu, Emma Gerald.

Alipoulizwa sababu za kifo hicho, Simwanza alisema yeye si msemaji wa kina kuhusu chanzo na alidai kuwa mara ya mwisho aliwasiliana naye siku mbili zilizopita kwa ujumbe wa simu ya mkononi.

“Kuumwa kweli alikuwa anaumwa, hasa kipindi cha kesi yake magonjwa ya hapa na pale ikiwamo presha. Si unajua mambo ya kesi hayana mwenyewe, lakini baada ya kesi kumalizika tulikuwa tunataniana kwamba sasa nina imani utakuwa poa kwani kila kitu kipo sawa,” alisema Simwanza.

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha alisema waliupokea mwili wa Masogange saa 12:20 jioni. “Tumeupokea na kwa sasa upo kwenye chumba chetu cha kuhifadhia maiti,” alisema Aligaesha.

Hivi karibuni, Masogange alihukumiwa kulipa faini ya Sh1.5 milioni na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kukutwa na hatia ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin, alibainika kutumia dawa hizo kati ya Februari 7 na 14, 2017, alilipa faini akaachiwa huru.

Kabla ya tukio hilo, Julai, 2013 Masogange na mwenzake Melissa Edward walikamatwa na mabegi mawili makubwa yaliyokuwa na kemikali bashirifu aina ya Crystal Methyl Amphetamine katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo nchini Afrika Kusini.

Mahakama ya Kempton ya Afrika Kusini iliwahukumu wawili hao kifungo cha miezi 30 au kulipa faini ya Randi 15,000 (sawa na Sh2.4 milioni) kutokana na kosa hilo, ambapo walilipa na kuachiwa.

Masogange alizaliwa Septemba 8, 1989 na pamoja na kujulikana zaidi kwa jina la Video Queen lakini amewahi kuonekana katika nyimbo za Belle 9 (Masogange) Gubegube wa Barnaba na Msambinungwa wa Tunda Man.

No comments:

Post a Comment

Popular