Spika wa Bunge afunguka kuhusu gharama za Matibabu ya Tundu Lissu. - KULUNZI FIKRA

Friday, 20 April 2018

Spika wa Bunge afunguka kuhusu gharama za Matibabu ya Tundu Lissu.

 
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Mhe Job Ndugai amesema ili matibabu ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Mhe Tundu Lissu yagharamiwe na Bunge anapaswa kuwa na vibali vya aina tatu na kwamba anajua watu wa Ujerumani wanamsaidia.

Spika Ndugai alisema hayo bungeni Jana alipojibu mwongozo wa mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliyehoji sababu za Lissu anayetibiwa nchini Ubelgiji kutogharimiwa na Serikali kama ilivyo kwa wabunge wengine, akiwamo Spika.

Mhe Lissu alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya hadi Januari 6 alipohamishiwa Ubelgiji katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven anakoendelea na matibabu.

Tangu wakati huo familia ya Mhe  Lissu na viongozi wa Chadema wamekuwa wakilalamikia Bunge kutogharimia matibabu yake, huku mbunge huyo mara kadhaa akizungumzia jambo hilo.

Mhe Lema katika mwongozo wake alisema, “Wakati Bunge la Bajeti likiendelea na vikao vyake mbunge mwenzetu yupo Ubelgiji na ofisi ya Spika bado inakataa kumlipia matibabu yake na haki zote za kimsingi anazo kama wewe (Spika) ulipokuwa India kufanyiwa matibabu na check-up (uchunguzi) Serikali iligharamia matibabu yako.”

Katika majibu yake, Mhe  Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa (CCM) alisema mbunge anaweza kutibiwa nje ya nchi kwa njia mbili; binafsi au kwa gharama za Bunge zinazoidhinishwa na Serikali.

Spika Ndugai alisema hoja ya Mhe  Lema imemlenga yeye moja kwa moja na kumtaka wakati mwingine kujenga hoja iliyosimama na kusisitiza kuwa katika matibabu hakuna anayestahili na asiyestahili.

Spika Ndugai alisema kwa mbunge kutibiwa nje, ili hundi iandikwe ni lazima kuwe na barua yenye kibali cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwamba mgonjwa huyo anahitaji rufaa na nchi ipi apelekwe; kibali cha Wizara ya Afya na lazima Spika atoe barua ya kibali kutoka kwa Rais.

“Nikishapata hivi vitatu ndipo mhasibu wa Bunge anaweza kuandika hundi kwa mbunge yeyote kwenda kutibiwa nje ya nchi,” alisema Spika Ndugai.

“Mhe Lema wakati Mhe Lissu anashambuliwa hukuwepo, wenzako walimpeleka Nairobi wakiwa na mwakilishi wa familia yake na viongozi wako (Mchungaji Peter- mbunge Iringa Mjini) Msigwa na Kiongozi wa Kambi (ya upinzani bungeni - Freeman Mbowe) ambao ni wajumbe wa kamisheni. Uamuzi wa kumpeleka Nairobi ulikuwa binafsi,” alisema Spika Ndugai.

Aidha, Spika Ndugai alisema wapo wabunge wengi ambao wanatibiwa kwa gharama zao binafsi, akiwamo mbunge wa Misungwi (CCM), Mhe Charles Kitwanga aliyesema kuwa alimuaga wakati akielekea Ujerumani kwa matibabu.

Ilani ya CCM

Wakati huohuo, Spika Ndugai ameiagiza Ofisi ya Katibu wa Bunge kuhakikisha wabunge wote wanapatiwa nakala za Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa maelezo kuwa wapo wa upinzani ambao hawana uelewa kuhusu ahadi za chama hicho tawala ilizozitoa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Spika Ndugai alisema hayo akijibu mwongozo wa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe Kangi Lugola aliyeomba mwongozo kutokana na mbunge wa Buyungu (Chadema), Mhe Kasuku Bilago kuhoji sababu za Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, aliyedai amekuwa akiwadanganya wananchi kuwa fedha za mpango wa kunusuru kaya maskini chini ya Tasaf zinatolewa na chama hicho tawala.

Mhe Lugola alisema kumekuwa na upotoshaji unaofanywa na wabunge wa upinzani ambao wanaonyesha dhahiri kutoifahamu Ilani ya CCM na shughuli zinazofanywa na Polepole.

“Nakubaliana na wewe (Lugola) kwa asilimia 100. Katibu angalia uwezekano wa kupata nakala hizo kwa wakati mwafaka na kama ni chache, basi uhakikishe upande huu wa kushoto (eneo la wapinzani) wapewe kipaumbele. Wataelewa chama tawala kinafanya nini ili isilete mkanganyiko", alisema Mhe Lugola.

No comments:

Post a Comment

Popular