Serikali yatenga Trilioni 1.5 kwaajili ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa. - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 24 April 2018

Serikali yatenga Trilioni 1.5 kwaajili ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa.

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeomba kuidhinishwa Sh4.2trilioni kwa mwaka wa fedha 2018/19, na kati ya fedha hizo, Sh1.5 trilioni zimepangwa kutumika kujengea reli ya kisasa (SGR) na huku Sh495 bilioni kwa ajili ya kununulia ndege mbili za abiria.

Akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni Mjini Dodoma Jana, Waziri Profesa Makame Mbarawa alisema itakuwa na utekelezaji wa ujenzi wa barabara na madaraja, ukarabati na ujenzi wa viwanja vya ndege na ununuzi wa vivuko vipya.

“Serikali imetenga Sh1.5 trilioni ambazo ni fedha za ndani kuendelea na ujenzi wa reli ya kati ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro (kilomita 300) na Morogoro hadi Makutupora (kilomita 422) na Sh1.4trilioni zitatumika,” alisema Profesa Mbarawa.

“Sh100 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli ya Isaka-Rusumo (kilomita 71) kwa kushirikiana na Serikali ya Rwanda.” alisema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa alisema Sh3 bilioni zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kumwajiri mtaalamu atakayeandaa nyaraka za kusaidia kutafuta fedha za ujenzi wa reli ya Mtwara-Mbambabay na matawi ya Mchuchuma na Liganga na Sh1.5 bilioni zitakamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi wa njia mpya za reli jijini Dar es Salaam.

Pia Profesa Mbarawa alisema mpaka sasa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa kuanza na sehemu ya Dar es Salaam-Morogoro na Morogoro-Makutopora utekelezaji wake umefikia asilimia 10 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 2019.

Kuhusu ndege, Profesa Mbarawa alisema mwaka 2018/19 ATCL imetengewa Sh495 bilioni kununua ndege mbili; moja aina ya Bombardier Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76 na ndege kubwa ya masafa marefu aina ya Boeing 787-8 (Dreamliner) yenye uwezo wa kubeba abiria 262.

“Fedha hizo pia zitatumika kulipia gharama za uendeshaji wa ndege, mafunzo ya marubani, wahandisi na wahudumu pamoja na ulipaji wa madeni,” alisema Profesa Mbarawa.

Aidha Profesa Mbarawa alisema mwaka 2018/19, Serikali imepanga kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 597.10 kwa kiwango cha lami, ujenzi wa madaraja 15 pamoja na ukarabati wa kilomita 72.10 kwa kiwango cha lami katika barabara kuu.

“Wakala wa barabara umepanga kufanya matengenezo ya barabara kuu na barabara za mikoa ambayo yatahusisha matengenezo ya kawaida kwa kilomita 32,653, matengenezo ya muda maalumu na sehemu korofi kilomita 6,292, na matengenezo ya madaraja 3,281,” alisema Profesa Mbarawa.

Miongoni mwa barabara hizo ni ile ya Dar es Salaam-Chalinze-Morogoro hadi Dodoma ambako mradi huo umetengewa Sh9.3 bilioni kwa ajili ya kulipa madai ya mshauri mwelekezi anayefanya upembuzi yakinifu.

Pia Profesa Mbarawa, alizungumzia kutengwa kwa Sh19.5 bilioni kwa ajili ya kuanza upanuzi wa sehemu ya barabara ya Morocco-Mwenge jijini Dar es Salaam na uboreshaji wa mifereji ya maji ya mvua katika barabara ya Mwenge-Tegeta.

“Ujenzi wa madaraja makubwa umetengewa Sh46 bilioni zinazohusisha kuanza kwa ujenzi wa daraja la Selander (Dar es Salaam), New Wami (Pwani), Msingi (Singida), Sukuma na Simiyu (Mwanza),” alisema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa alisema katika bajeti hiyo, Sh215 bilioni zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege.

Vile vile Profesa Mbarawa alisema ujenzi huo utahusisha viwanja vya ndege vya Kigoma, Bukoba, Mpanda, Tabora, Songwe, Msalato, Shinyanga na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Mwanza, Arusha, Mtwara na Kilimanjaro.

“Sh13 bilioni zitatumika katika ujenzi wa vivuko na maegesho ya vivuko, ikiwemo upanuzi wa maegesho ya Kigamboni, ununuzi ya kivuko kipya cha Magogoni na ukarabati wa vivuko vya MV Pangani, MV Sengerema, MV Kigamboni na MV Misungwi,” alisema Profesa Mbarawa.

Waziri huyo alisema kwamba kati ya fedha zinazoombwa na wizara hiyo, Sh1.8 trilioni ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi, Sh2.3 trilioni kwa ajili ya ile ya uchukuzi na Sh18 bilioni sekta ya mawasiliano.

No comments:

Post a Comment

Popular