Rais Magufuli ataka mabadiliko ndani ya Jeshi la polisi. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 8 April 2018

Rais Magufuli ataka mabadiliko ndani ya Jeshi la polisi.

 
Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania Dkt   John  Pombe Magufuli amemwaga neema kwa Jeshi la Polisi nchini, baada ya kutangaza kutoa Sh bilioni 10 za ujenzi wa nyumba za askari wa hali ya chini na pia kuahidi ajira 1,500 kwa vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Lakini akalitaka jeshi hilo libadilike upya, huku akipiga marufuku Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Naibu wake, Katibu Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, makamanda wote wa Polisi wa Mikoa, pamoja na askari kujihusisha na kufyeka mashamba ya bangi.

Rais Magufuli alitangaza hayo jana kwenye Uwanja wa Shehe Amri Abeid jijini hapa wakati alipozungumza na viongozi mbalimbali wa Jeshi la Polisi, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama sanjari na wananchi katika kumbukizi ya kifo cha Mzee Abeid Amani Karume iliyoenda sambamba na maonesho ya kazi za polisi. Alisema ameamua kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa askari wa chini ambao maisha yao na kazi wanazofanya hayaendani na maana halisi ya jeshi hilo.

Alisema anajua changamoto za askari polisi walizonazo kwani mkewe Mama Janeth Magufuli amelelewa katika mazingira hayo ya chini wakati baba yake mzazi akiwa askari. Alisema fedha hizo alizozitoa zitawezesha ujenzi wa nyumba za askari hao ili wafanye kazi kwa weledi kwani kazi za polisi ni ngumu zinazohitaji kutokuwa na msongo wa mawazo katika kuhudumia jamii.

Pia alimwagiza IGP Sirro kumpa mapendekezo ya maofisa wa polisi anaotaka wapandishwe vyeo na kuonya wakuu wa vitengo vya polisi kuacha upendeleo na wawapandishe vyeo watu wanaostahili kupandishwa vyeo badala ya kupandisha mtu asiyestahili.

“Ninafanya hivi kwa sababu ninathamini kazi za polisi na mtembee kifua mbele na achaneni na maneno ya watu, bali fanyeni kazi na amueni yale mnayoona yanafaa kwa usalama wa wananchi na mali zao,” alisema.

Kuhusu bangi, alisema anashangaa kuona askari wanafyeka bangi na kuagiza mara moja kuanzia Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, makamanda wa Polisi na askari polisi wasifyeke mashamba ya bangi, badala yake wawashike wanavijiji wote na waende mashamani wafyeke bangi kisha wachome. “Polisi kutumika kuchoma bangi au kufyeka ni kuaibisha jeshi kwa kufyeka bangi na kuna siku nimemuona waziri naye anafyeka bangi nikashangaa.

Nasema sitaki kuona polisi wanafyeka bangi, badala yake shikeni kijiji kizima kifanye kazi hiyo,” alisema Rais Magufuli na kuongeza: “Mkifyeka bangi wananchi wataendelea kulima tu na nisiwaone mnaenda kukata bangi hadi polisi wa chini msikate bangi, wakamate wananchi wenyewe hata kama kuna mawe wayaviringishe hadi wataacha wenyewe.”
Akizungumzia kuhusu mauaji yaliyotokea Kibiti mkoani Pwani, Rais Magufuli alisema mauaji hayo yalisababisha watu 59 kuuawa wakiwemo raia 42 na askari 17, na jambo la kushangaza miongoni mwa waliouawa, walikuwa ni raia pamoja na viongozi wa CCM.

“Najua yawezekana wabaya hao bado wapo, lakini nawaambia endeleeni kufanya kazi na yale mtakayoamua amueni na nitawasapoti,” alieleza Rais Magufuli huku akilitaka jeshi hilo kurekebisha upungufu wao na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaolichafua.

Akizungumzia uzinduzi wa nyumba 31 za Polisi, aliwapongeza wafanyabiashara William Chambulo na Lodhia Group pamoja na wafanyabiashara wengine wakiwamo wakurugenzi wa Kampuni ya TanzaniteOne walioshirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kujenga nyumba hizo za askari na vituo viwili vya polisi Arusha.

Alihoji kuwa kama Mkuu wa Mkoa wa Arusha amewahamasisha wafanyabiashara kujenga nyumba hizo kwa muda mfupi, ni kwa nini wakuu wengine wa mikoa wasiige hilo, pamoja na wabunge kupitia Mfuko wa Jimbo?

Akizungumzia maendeleo ya wananchi, Rais Magufuli  alisema wameimarisha ulinzi na usalama sanjari na ongezeko la ukusanyaji wa mapato kwani hadi kufikia Desemba 2017, serikali ilikusanya Sh trilioni 1.7 Alimpongeza Gambo na wadau wengine kwa kuanzisha viwanda mbalimbali na kusisitiza kuwa palipo na amani kila kitu kinawezekana.

Alisema Arusha ilifika mahali watu hawataki kuja na akaagiza Polisi iendelee kudhibiti wanaoharibu amani ya Arusha. Aidha, alimpongeza Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro kwa kupenda maendeleo lakini akakataa ombi la kufidiwa ng’ombe waliokufa kwa ukame kwa kuwa hivi sasa hali ya hewa ni nzuri kwa malisho.

Akasema yeye hatatoa ng’ombe wilayani Longido na kumweleza Mbunge wa jimbo hilo, Dk Stephen Kiruswa kuwa kama Rais, amepeleka mradi wa maji mkubwa wilayani humo, lakini ng’ombe hatatoa.

Pia alitumia hadhara hiyo kumwombea kwa dakika Mzee Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar, aliyeisaidia Zanzibar kuleta mapinduzi kwa ajili ya ukombozi wa Zanzibar. Naye IGP Sirro alisema wale wenye nia ya kuchafua amani ya nchi waache mara moja na kama wanaona ushauri huo hauna maana, basi wasije laumiana baadaye.

Alimpongeza Rais Magufuli aliyetoa Sh milioni 250 kujenga nyumba za askari 14 zilizoungua Septemba 27, mwaka jana na Jeshi la Polisi likatoa Sh milioni 40. Alishukuru Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Arusha sanjari na wafanyabiashara waliowezesha nyumba 18 za polisi kujengwa kwa gharama ya Sh milioni 550 kwa ujumla.

Kabla ya kwenda uwanjani, Rais Magufuli alifungua Kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia kilichopo karibu na eneo ambalo nyumba hizo za polisi zilijengwa baada ya kuungua kwa moto mwaka jana. Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Makazi ya Polisi, Richard Malika, kituo hicho kipya cha diplomasia kitakuwa kikitoa huduma mbalimbali za kidiplomasia.

Pia kitakuwa na kikosi cha Idara ya Uhamiaji na ndani yake kitakuwa na polisi waliopewa mafunzo maalumu ya kuhudumia mambo ya diplomasia. Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema Watanzania wanahitaji maendeleo na asitokee mtu anayetaka kuharibu amani hivyo ni vyema wananchi wakapata maendeleo hayo kwa amani.

No comments:

Post a Comment

Popular