Rais Magufuli ametoa maagizo kwa Tanesco. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 4 April 2018

Rais Magufuli ametoa maagizo kwa Tanesco.

 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe  Magufuli ameitaka Wizara ya Nishati kuanza kufi kiria kushusha gharama za umeme. Amesema hatua hiyo itawezesha wananchi wengi, kuunganishwa kwenye nishati hiyo na kuitumia.

Magufuli alisema hayo Dar es Salaam jana, wakati akizindua Kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi II chenye uwezo wa kuzalisha megawati 240 za umeme, ambazo zinaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa. Alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2015/16, asilimia 36.6 tu ya Watanzania ndiyo wameunganishiwa huduma ya umeme, ingawa sasa asilimia hiyo inaweza kufikia asilimia 40.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, asilimia 60 ya Watanzania hawajaunganishwa kwenye nishati hiyo na badala yake wanaendelea kutumia kuni, mkaa na mafuta ya taa, kwa kuwa bei ya umeme iko juu na wengi hawaimudu.

“Athari za kutumia kuni na mkaa zinafahamika; kwanza zinachangia kuharibu mazingira, ambapo kwa nchi yetu inakadiriwa kuwa kila mwaka huwa tunapoteza hekta 400,000 za misitu; lakini pia tunatambua bei ya umeme wetu bado iko juu,” alieleza Magufuli. Alisema mahitaji ya umeme sasa ni megawati 1,400 na ukijumlisha megawati uzalishaji sasa ni megawati 1,513.3, mafanikio makubwa.

Kutokana na mipango iliyopo ya serikali ya kuongeza vyanzo vya kuzalisha umeme ili kufikia megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020, Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Nishati kuanza kufikiria kupunguza gharama za nishati hiyo ili wananchi wengi waweze kuimudu.

Uwezo na gharama za Kinyerezi II Ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi II, ulizinduliwa Machi, 2016 na umekamilika siku 45 kabla muda uliopangwa. Rais Magufuli aliishukuru Kampuni ya Kijapani ya Sumitomo Corporation, iliyojenga mradi huo, kwa kuukamilisha kwa wakati na kwa viwango.

Alisema mitambo hiyo ya Kinyerezi II ni ya kipekee kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na ina uwezo wa kuzalisha megawati 240. Sababu za kukamilika mapema kwa mradi huo, zimeelezwa ni utayari wa serikali kutoa Sh bilioni 120 na mkopo wa gharama nafuu kutoka Japan wa Dola za Marekani milioni 292.4.

Hivyo gharama yote kufikia Sh bilioni 758, sawa na dola za Marekani milioni 344. Upanuzi wa miradi mingine ya umeme Serikali imesema mbali na mradi wa Kinyerezi II, upanuzi wa Kinyerezi I utakaozalisha Megawati 325 kutoka Megawati 150 za sasa unaendelea.

Rais Magufuli alisema mradi huo unatekelezwa na serikali kwa gharama ya Sh bilioni 400 na utakamilika mwakani mwanzoni. Miradi mingine iliyo hatua mbalimbali ya utekelezaji wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ni Kinyerezi III wa megawati 600. Mingine ni Kinyerezi IV megawati 330, Mtwara megawati 300, na mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorgewa megawati. 

Rais Magufuli alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya kuzalisha umeme vya gesi asilia, upepo, maji, jua, makaa ya mawe na nyuklia. Uzalishaji, Usafirishaji na Usambazaji umeme Ili umeme uweze kufika kwa wananchi, Rais Magufuli alisema ni lazima upitie hatua tatu muhimu za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji.

Alisema hatua zote hizo zina changamoto zake. Alisema hivi karibuni serikali imekamilisha mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga kwa kilomita 632, Singida hadi Namanga msongo wa kilovoti 400 kwa umbali wa kilomita 414. Miradi mingine iliyokamilika ni ule wa kutoka Mbeya hadi Nyakanazi wa kilovoti 400 na Makambako hadi Songea wa kilovoti 250.

Kuhusu miradi ya kusambaza umeme, Magufuli alisema hivi sasa kuna mradi mkubwa wa kupelekaumeme vijijini awamu ya tatu. Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020/21, vijiji vyote nchini viwe vimefikiwa na miundombinu ya umeme. Alisema hadi kufikia Desemba 2016, vijiji 4,395 kati ya vijiji 12,268 vilifikiwa na miundombinu ya umeme na vilivyobaki sasa ni vijiji 7,873 tu.

Ajira Kutekelezwa kwa mradi huo wa Kinyerezi II, kumesaidia kutoa ajira kwa Watanzania wengi. Kati ya wafanyakazi zaidi ya 2,000 walioajiriwa na kampuni iliyojenga mradi huo, asilimia 95 ni Watanzania, hivyo fedha nyingi kubaki nchini. Taasisi zaonywa Pamoja na mafanikio hayo ya miradi ya umeme, Rais Magufuli alizionya taasisi za serikali kuacha kukwamishana kutekeleza miradi ya maendeleo.

Rais Magufuli alisema hayo baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Dk Titus Mwinuka kusema changamoto kubwa ni kodi na tozo mbalimbali, wanazokumbana nazo kutoka taasisi nyingine za serikali, ambazo zinaongeza gharama za mradi wanaotekeleza.

Kodi na tozo hizo, zimeongeza gharama za mradi kutoka dola za Marekani milioni 344 hadi dola za Marekani milioni 356.2. Rais alizitaka taasisi za serikali kushirikiana, badala ya kukwamishana. Ubalozi Japan Mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini, Hiroyuki Kubota alisema mradi huo umejengwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na usalama.

Pia Rais Magufuli alisema serikali ya Japan, inaunga mkono sera ya kuwa na uchumi wa viwanda ya Tanzania. Alisema uhakika wa umeme unawezesha kufanikiwa sera hiyo ya viwanda, kuharakisha ukuaji wa uchumi na huduma nyingine nchini.

Waziri wa Nishati Kabla ya kumkaribisha Rais Magufuli, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema lengo la serikali ni kuzalisha megawati 5,000 za umeme ifikapo mwaka 2020 na megawati nyingine 10,000 ifikapo mwaka 2025. Viongozi mbalimbali walihudhuria uzinduzi huo wakiwemo mke wa Rais Magufuli, Mama Janeth, mawaziri, naibu mawazirina Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

No comments:

Post a Comment

Popular